Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatenga fedha kujenga soko la kisasa Ikungi?
Supplementary Question 1
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; lakini pia naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, changamoto iliyopo hapo Ikungi ni sawa sawa na iliyopo katika Jimbo la Singida Kaskazini katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo tulisha wasilisha maandiko kwa ajili ya kupatiwa soko la kisasa katika mji wa Melya njia panda ya Melya lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.
Je, Serikali inatoa commitment gani kwa ajili ya kujenga soko hilo la kisasa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi?
Swali la pili, Mji wa Ikungi pamoja na Singida Kaskazini hazina stendi zinazoeleweka za kisasa kwa ajili ya magari kuingia na kutoka. Je,Serikali sasa itajenga lini stendi hizo kwa ajili ya kupendezesha miji yetu lakini pia hata kuingizia mapato halmashuri zetu?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Igondo Ramadhani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ambayo pia iko katika Jimbo la Singida Kaskazini Halmashauri ya Singida la kukosa soko, na niwapongeze Halmashauri ya Singida kwa sababu tayari kweli walishawasilisha andiko mkakati kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa Ikungi pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwamba Serikali inaendelea na uchambuzi wa maandiko yale kuona kama yanakidhi vigezo vya kuwa miradi ya kimkakati ili fedha ziweze kutafutwa kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na changamoto ya stendi ya mabasi, Serikali imeshaweka mpango kazi kwenye halmashauri zetu zote kuanza kuainisha maeneo ambayo yanatakiwa kujenga stendi lakini pili kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani pamoja na Serikali kuu kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga maeneo hayo. Kwa hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Stendi hizo zinajengwa, ahsante.
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatenga fedha kujenga soko la kisasa Ikungi?
Supplementary Question 2
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa uko mradi wa TACTIC wa kujenga soko la kisasa pale Ipembe lakini na soko la vitunguu. Nataka kujua ni lini mradi huu utatekelezwa ili wananchi waweze kupata huduma stahiki?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa TATCTIC una awamu tatu. Awamu ya kwanza tayari iko hatua ya kutafuta wakandarasi, awamu ya pili iko hatua ya usanifu wa mwisho na awamu ya tatu itafanyiwa usanifu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kabla ya mwaka 2025 Serikali imeweka commitment kuhakikisha kwamba miradi yote ya TACTIC itakuwa imekamilika kwa sehemu na mingi iko kwenye utekelezaji hatua za mwisho, ahsante.
Name
Mohamed Lujuo Monni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chemba
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatenga fedha kujenga soko la kisasa Ikungi?
Supplementary Question 3
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mji wa chemba unakuwa kwa kasi lakini hauna soko kabisa. Naomba kujua mkakati wa Serikali wa kujenga soko pale kwenye mji wa Chemba, ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Monni Mbunge wa Jimbo la Chemba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekeze Mkurugenzi wa halmashauri ya Chemba kuainisha na kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko na kuleta andiko la kuona uwezo wa halmashauri kwa mapato ya ndani yanafikia eneo gani ili Serikali Kuu iweze kuona sehemu gani inahitaji kuchangia ili kujenga soko katika mji huu wa Chemba, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved