Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza: - Je, Serikali ipo tayari kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumiwa na Watu wenye Ulemavu wakati wa kuingia nchini?
Supplementary Question 1
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini kwanza kabla ya swali langu nitoe utangulizi, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema msamaha wa kodi uliotolewa ni baiskeli pamoja na magari mahususi kwa matumizi ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlemavu wa macho au asiyoona hivi gari lake linafananaje? Naomba kuuliza swali la kwanza; Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inatoa msamaha wa kodi kwa watu wenye ulemavu wa macho na vifaa vingine vyote wanavyoleta iwe sawa kama wale wenye ulemavu wengine waweze kupata msamaha wa kodi hiyo na kuleta unafuu wa maisha yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kumekuwa na baadhi ya Watendaji wa Wizara hiyo ambao wanahusika na utoaji wa msamaha wa kodi wakiwatoza kodi wenye ulemavu na katika majibu ya Mheshimiwa Waziri ameonyesha msamaha wa kodi unatolewa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari nimletee watu wenye ulemavu ambao wametozwa kodi wakati wanahitaji msamaha huo? (Makofi)
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tendega, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu maswali hayo, naomba nimpongeze sana kwa kiasi ambacho anawapigania ndugu zetu wenye ulemavu. Swali lake la kwanza kama nilivyojibu katika swali la msingi ni vifaa tu mahususi ambavyo wanatumia ndugu zetu wenye ulemavu ndivyo ambavyo vinapata msamaha, lakini maoni yake tunayachukua, tunaenda kuyaangalia kama yanaleta tija kwa pande zote mbili kwa walengwa na Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, siwezi kukataa kukutana na ndugu zetu, wananchi wenzetu wenye ulemavu na watu wengine wote mimi niko tayari kukaa nao, lakini naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu nikae na Mheshimiwa Mbunge tuone kwa kiasi gani tunaweza tukapata ufumbuzi wa suala hilo na kuwasaidia ndugu zetu hawa wenye ulemavu, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved