Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, lini mpaka wa Kasesya/Zombe utafanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo tunavyoongea mpaka ule unatumika lakini kwa kiasi kidogo sana na hili tatizo limetokana na upande wa pili wa Zambia ambapo wafanyakazi kama walivyo TRA Tanzania, ZRA wamekuwa hawaishi pale. Je, Serikali kwa kutumia ushirikiano uliopo na Zambia haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuongea na upande wa pili ili watumishi wa ZRA wawepo muda wote ili kusiwe na shida kwa wasafirishaji wa mizigo.

Swali la pili; ukitaka kwenda Congo ya Lubumbashi njia iliyokuwa rahisi kabisa ni kwa kupita Kasanga Port ambayo naomba niipongeze Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana. Kazi ndogo ambayo imebaki ni upande wa pili kwa maana kupitia Mlilo kule na kwa wakati huu ambao ni rahisi kabisa kutumia PPP.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kutangaza mradi huu ambao economically unaonekana kwamba viable? (Makofi)

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mpaka wetu wa Kasesya ambao una taasisi mbalimbali, kuna taasisi za Uhamiaji, Polisi, watu wa kilimo, TRA, kwa hiyo tunafanya kazi masaa 24, lakini upande wa wenzetu Zambia haufanyi kazi masaa 24, Serikali imechukua juhudi za kuwasiliana kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na hata mwaka jana tulifanya mikutano Tarehe 14 na 15 mwezi wa Kumi, kuhakikisha mpaka huu tunauhuisha na unafanya vizuri, waliahidi Serikali ya Zambia kwamba watafanya kama ambavyo tunafanya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekti, swali la pili kuhusu PPP hususan katika Bandari yetu ya Kasanga ambayo ni kweli imegharimu zaidi ya Bilioni 4.7 na Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumekuwa tukifanya mikutano mbalimbali kuishirikisha sekta binafsi ili upande wa pili wa Congo waweze kutengeneza barabara ili bandari yetu ya Kasanga Port iwe na tija. Kwa hiyo, haya tunaendelea kuyafanya, tunataendelea pia kuwasiliana na wenzetu wa Serikali ya Congo ili kuhakikisha miundombinu upande wa kwao inafanya vizuri, ahsante. (Makofi)

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, lini mpaka wa Kasesya/Zombe utafanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma?

Supplementary Question 2

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mpaka wa Namanga ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu lakini kuna msongamano mkubwa wa malori. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha huduma katika mpaka huu wa Namanga ili basi kuleta tija? Ahsante.

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na suala la mpaka wa Namanga kuwa na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna mipaka kama Tunduma pamoja na Namanga ni mipaka ambayo ina msongamano mkubwa na ni kwa sababu ya bidhaa zinazoingia na kutoka kwenda nchi jirani. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba kwanza maeneo haya tumepanga utaratibu na scanner ambazo ziko katika maeneo hayo, kabla zilikuwa zinafanya masaa 12 na sasa tumeweka mpango wa zifanye kazi masaa 24 maana yake usiku na mchana ili magari ya kwenda Kenya na magari ya kuingia Tanzania kusiwe na msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tumeweka eneo maalum kwa ajili ya kuegesha magari hususan ya mizigo ili yasisongamane sana eneo lile la mpakani, ahsante.

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: - Je, lini mpaka wa Kasesya/Zombe utafanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma?

Supplementary Question 3

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikumi idadi ya malori ni kubwa msongamano ule unasababisha hatari na usalama wa maisha ya raia na mali zao. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetoa Milioni Mia Moja kwa ajili ya kutatua tatizo hilo la malori kwa kutenga eneo na kusaidia ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini commitment ya Serikali kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika kutatua tatizo la malori ambalo linasababishwa na mizani pale Mikumi? (Makofi)

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F.
MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo la Mikumi kuna msongamano wa malori mengi na Mheshimiwa Mbunge ninakupongeza kwa kufatilia jambo hili, alipolileta Serikalini tukawapa eneo ambalo ni la TRC kwamba waendelee kulitumia na tayari tulishatoa kibali hicho kama Serikali, kinachosubiriwa sasa ni wao kama Halmashauri kulifanyia hilo eneo ukarabati ili malori yaliyoko pale barabarani yahamie eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninakupongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zako hizo. Ahsante.