Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH M. MASSABURI aliuiliza: - Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Maofisa Usalama Barabarani Falme za Kiarabu na Vietnam ili kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali?

Supplementary Question 1

MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wenzetu wa nchi hizo wamekuwa wakitumia sheria kali ambazo kila dereva anatii sheria na kunusuru maisha ya wananchi wao; je, ni lini Serikali itatunga sheria kali ambazo zitaweza kutusaidia kunusuru maisha ya Watanzania yanayopotea kutokana na ajali za barabarani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali imeshindwa kuwadhibiti madereva wa bodaboda ambao hupita kwenye makutano bila kuzingatia taa za barabarani na hatimaye kusababisha ajali na kusababisha watu kufariki na kuleta walemavu wengi katika nchi yetu? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, juu ya sheria ya usalama barabarani iliyo kali zaidi; naamini Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu kwamba tulishawasilisha hapa sheria ikasomwa kwa mara ya kwanza na kwa busara ya Bunge lako Tukufu ilitakiwa irudishwe kwa ajili ya kuboresha maeneo ambayo yalikuwa na changamoto. Napenda kumhakikishia kwamba uboreshaji uko hatua za mwisho, katika Mabunge yajayo tunatarajia iletwe hapa ili Bunge likiridhia tuwe tumemaliza eneo hilo la sheria kali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kushindwa kuwadhibiti bodaboda; hatujashindwa. Tulichojifunza ni kwamba hawa vijana namna wanavyoingia kwenye uendeshaji ni kwamba wengine hawajapata kabisa mafunzo. Jeshi la Polisi, hususan Kitengo cha Usalama Barabarani, wameanza na hatua za kuwafundisha.

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sasa hivi wamewekwa kwenye makundi katika maeneo mbalimbali wanayopangwa katika vikundi. Katika makundi yao yale wanapata mafunzo, traffic police na wenye vyuo vya udereva wanakwenda wanawasomesha ili wajue taratibu za usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, wale wanaokiuka hatua zinachukuliwa. Ndiyo maana tukienda maeneo ya polisi mtakuta pikipiki nyingi ziko kule za wale waliokiuka sheria. Tutaendelea kujenga uwezo wao na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka. Kupitia Bunge lako, nielekeze traffic police wasiwe na muhali na vijana hawa ambao wanakaidi sheria makusudi, hasa wanaopita kwenye taa za barabarani wakati zimezuia, nashukuru.

Name

Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH M. MASSABURI aliuiliza: - Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Maofisa Usalama Barabarani Falme za Kiarabu na Vietnam ili kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali?

Supplementary Question 2

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa madereva wenye uzoefu na ujuzi wa udereva kwa kuwa walikosa kigezo cha kuwa na cheti cha form four. Na kwa kuwa ajali zimekuwa nyingi katika nchi hii ambazo zinaleta ulemavu au walemavu wengi nchini: -

Je, Serikali haioni sasa sababu ya kuwarudisha madereva hao kazini kwa sababu cheti cha form four hakina uhusiano na ujuzi au utaalamu wa udereva? (Makofi)

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Mathew Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuwaondoa watumishi waliokuwa hawana vyeti vya form four wakiwemo madereva ilikuwa ni Sera ya Menejimenti ya Utumishi ambao tumeridhia wote kama nchi, kwamba tuna vijana waliokwisha soma mpaka kidato cha nne na kuendelea, ni vizuri utumishi wa umma uwazingatie hao na kuruhusu wale ambao walikuwa kwenye utumishi wa Umma wajiendeleze. Serikali bahati nzuri ilitoa muda maalum wa watu wale kujiendeleza, na walioshindwa kujiendeleza ndio waliondolewa.

Mheshimiwa Spika, wale wa darasa la saba waliojiendeleza wengi walibaki kwenye utumishi wa Umma. Nadhani bado hakuna hoja ya msingi ya kurejea darasa la saba wakati tunaowahitaji kwa mujibu wa sera yetu ni baada ya kidato cha nne, na vyuo vya udereva vipo ambapo hawazuii kuingia kupata mafunzo. Kwa hivyo tunalichukulia positively kwa maana kwamba wataendelea kujielimisha na wanaokiuka wanachukuliwa hatua, ahsante.

Name

Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Primary Question

MHE. JANETH M. MASSABURI aliuiliza: - Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Maofisa Usalama Barabarani Falme za Kiarabu na Vietnam ili kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali?

Supplementary Question 3

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, madereva wengi wa bodaboda hawana leseni kwa sababu ya gharama kubwa zinazotakiwa kwa ajili ya kupata leseni, na ndiyo maana wanaendesha pasipo kuwa na leseni. Sasa swali; kwa nini tusiweke utaratibu mzuri wa kuwafundisha pamoja kwa gharama nafuu ili waweze kufanya kazi hiyo kwa uzuri?

Name

Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vedastus Manyinyi Mathayo, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba katika baadhi ya maeneo ikiwemo kwenye jimbo lake, ameanzisha huo utaratibu, na sisi upande wa usalama wa raia tunaupokea.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwahamasisha maeneo mengine pia watumie utaratibu kama huu unaopendekezwa na Mbunge, kwamba wanapokuwa wengi katika chumba kimoja wakafundisha kwa gharama za chini, wakawekewa utaratibu nafuu wa kupata leseni zao ili kuepuka hao wanaokwepa kukata leseni kwa sababu ya gharama kubwa. Na bahati nzuri maeneo mengine wameruhusu kulipa leseni kidogo kidogo, kwa hiyo likifanyika hilo nadhani hakutakuwa na matatizo yoyote.