Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Primary Question

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: - Je, lini Jeshi la Uhifadhi litapata Kamishna Jenerali na kuleta muunganiko katika divisheni za NCAA, TANAPA, TAWA na TFS?

Supplementary Question 1

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Ni standard ya kawaida kwa taasisi zote za Serikali, lakini hasa majeshi, kuwa na kiongozi mkuu wa taasisi husika kwa ajili ya chain of command, lakini Jeshi la Uhifadhi halina kiongozi mkuu kwa maana ya divisheni zile TFS, TAWA, TANAPA, kila mtu ana-operate mwenyewe anavyoona inafaa. Sasa ikitokea viongozi wakuu wa nchi wanataka kuongea na majeshi wao Jeshi la Uhifadhi wanampeleka nani kuwawakilisha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kwamba wakiona changamoto wataanzisha mchakato wa kubadilisha sheria ili kupata kamishna. Anataka aone changamoto gani ilia one sasa kuna uhitaji wa kuwa na Commissioner General wa Jeshi la Uhifadhi? Ahsante.

Name

Mary Francis Masanja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi ni kwamba taasisi hizi zina majukumu tofauti. Ukiangalia utekelezaji wa majukumu yao unaendana sambamba na namna ambavyo majeshi haya yameundwa. Kwa mfano kwenye Taasisi za TANAPA na Ngorongoro, taasisi hizi zina baadhi ya vitu ambavyo vinaruhusiwa kutumika lakini kuna baadhi ya taasisi ambazo zinazuia kama TAWA na TFS.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye upande wa TAWA na TFS tunaruhusu masuala ya uvunaji na uwindaji wa kitalii. Kwa hiyo, utaona yale majukumu yenyewe ya taasisi yanatofautiana. Kwa hiyo, kila kamishna wa uhifadhi anatekeleza majukumu kulingana na muundo wa taasisi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa sasa hivi tunaona bado wanafanya kazi vizuri na wote wanaripoti kwa Katibu Mkuu, kwa hiyo mkuu wa nchi anapotaka kuzungumza na majeshi haya anazungumza na Katibu Mkuu ambaye ndio msemaji wa Wizara kwa upande wa utendaji.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa maoni yake, tunayapokea na pale ambapo tutaona kwamba kuna uhitaji sasa wa kuunda jeshi ambalo litakuwa na mwakilishi ambaye ni Kamishna Jenerali, basi tutafanya hivyo na tutapitia kanuni zetu ili tuendane sambamba na majeshi yaliyopo.