Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Hospitali ya Haydom inahudumia Mikoa ambayo umeitaja ya Singida, Simiyu, Arusha, Dodoma na Mara; na nashukuru Serikali kwa kutoa fedha na kupanga kiwango hiki cha shilingi milioni 570.
Je, kwa kuwa Serikali sasa imesema haya na hela iliyopelekwa ni kidogo, haioni sasa ni muda wa kuongeza ruzuku hii ili hospitali hii ikaweza kutoa huduma nzuri kwa watu wanaozunguka?
Swali la pili, kwa kuwa tumeleta maombi ya hospitali hii kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Kikanda na kwa kuwa Wabunge wanaozunguka hospitali hii na Mikoa niliyoitaja tumeomba namna hiyo.
Je, ni lini sasa Serikali itajibu maombi haya ya kuipandisha Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Kanda?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba hospitali hiyo ikiwezeana iongezewe ruzuku; kwanza naomba niwapongeze watu wote wa Mkoa wa Manyara kuanzia wewe, Mheshimiwa Jitu Soni, Kaka yangu pale, wote mnafanya juhudi kubwa kwa ajili ya Mkoa wenu wa Manyara, lazima niwapongeze. Mara nyingi mmefika katika ofisi yangu suala la kutaka madaktari, kutaka nini, inaonekana mnajali shida za wananchi wenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo ndiyo maana nimesema Serikali iko katika mchakato wa kuweka mkataba vizuri, kwa sababu hospitali hii sasa hivi huduma kubwa ilikuwa inatokea Kiwilaya, lakini sasa hivi ruzuku ya mishahara zaidi ya shilingi milioni 500 kwa sasa, na zile za madawa zaidi ya shilingi milioni 134, na kwa mwaka huu wa fedha ambao tunaendelea nao, tutawapatia ruzuku ya shilingi milioni 714 mishahara peke yake, vivyo hivyo katika dawa kutoka shilingi milioni 130 tunakwenda mpaka zaidi ya shilingi milioni 300, maana yake tunazungumza suala la shilingi bilioni moja. Hivyo, Serikali imeshaona jinsi gani sasa Hospitali hii ya Haydom inatakiwa ipewe kipaumbele, kwa hiyo tumeshaiweka katika mikakati. Tunachokifanya sasa hivi ni kusubiri suala ule mkataba ufanyiwe vetting utaratibu ukishakamilika basi nadhani suala zima la ruzuku litakwenda vizuri kama linavyokusudiwa Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kupandisha hadhi, naamini kwa sababu suala la kupandisha hadhi ni mchakato mzuri na naamini katika kikao cha RCC nitamaliza hilo lipo katika Ofisi ya Waziri wa Afya, litapitiwa. Mwisho wa siku suala la Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Kanda itafanyiwa hivyo. Serikali lengo lake kubwa ni kuboresha maisha ya wananchi wake na hususan kuboresha sekta ya afya. Kwa hiyo, kwa sababu mchakato huu wote ulishakamilika na Wizara ya Afya, mwisho wa siku tutapata majibu halisia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa Manyara wanapata huduma bora.

Name

Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?

Supplementary Question 2

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kwa kuwa, fedha za own source hazitoshi wakati mwingine kulipa hata posho za Madiwani, ni kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Dongobesh ili kuondoa msururu mkubwa katika Hospitali ya Haydom kwa ajili ya wananchi wa Mbulu Mjini na Mbulu Vijijini?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupandisha Kituo cha Afya cha Dongobesh sisi hatuna matatizo, provided kwamba vigezo vimefikiwa. Ule mchakato Mheshimiwa Ester ninakuamini kwa sababu umenisaidia sana, hata Mzee pale alinisaidia sana, miongoni mwa watu walioshiriki nilivyokwenda katika Shule ya Kisimani pale katika Jiji la Arusha. Kwa hiyo najua ni mpiganaji na unapambana katika mambo mbalimbali. Na mchakato huu mkimaliza mchakato katika vikao vyenu, katika ule utaratibu wa kawaida, maana kuna hilo, lakini ukienda kwa Mheshimiwa Jitu Soni pale, kituo cha Afya cha Magugu na wao wanaomba ipandishwe ifike katika hadhi inayokusudiwa.
Naomba maombi haya sasa yaende pamoja Wizara ya Afya, yakifika Wizara ya Afya naamini Dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwa sababu anajali sana haki na matatizo ya akina mama na watoto jambo hili ataliangalia kwa jicho la karibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya, vituo vya afya vinavyotaka vipandishwe viwe katika hadhi inayokusudiwa au katika zahanati kupandishwa kuwa vituo vya afya, provided kwamba vigezo zimefikiwa Serikali haitoshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, naomba niwasisitize kwamba vile vikao vya awali vikishakaa lazima mchakato uende kama unavyokusudiwa katika Wizara ya Afya na mwisho wa siku Serikali itafanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wananchi wake.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?

Supplementary Question 3

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbulu yenye majimbo mawili, tuna vituo vya afya ambavyo havijakamilika takribani vituo vitano. Kwa mfano, Tarafa ya Nambisi ina kituo cha afya ambacho hakina hadhi, Tarafa ya Daudi na Tarafa ya Dongobesh.
Je, ni kwa nini Serikali isichukue hatua za makusudi kukagua vituo vyote vya afya, na kwa kuwa Waheshimiwa Madiwani katika bajeti ya Halmashauri hawawezi kupitisha bajeti ikaenda kwenye kituo kimoja ili Serikali itenge fedha za kutosha kwa kila Halmashauri, kwa kila mwaka walau kuwa na kituo cha afya kitakachotengewa fedha kutoka Hazina, nje ya bajeti ya Halmashauri? Ahsante.

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa hoja muhimu sana ambayo ni muhimu sana imesaidia kuibua mambo mbalimbali, Mheshimiwa Zacharia alikuja pale ofisini, na alizungumzia suala zima la maboma ambayo yapo katika Jimbo lake ambayo hayajakamilika.
Ninakushukuru Mheshimiwa Mbunge, ulivyokuja pale ofisini siku ile na Mheshimiwa Jitu na Mheshimiwa Issaay pamoja, katika suala zima la maboma pia suala zima la watendaji, miongoni mwa hoja ambazo mmenisaidia ni kuweza kuangalia tutafanya vipi sasa tuweze kumaliza maboma.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili nimezungumza wiki iliyopita tumeelekeza Halmashauri zote zibaini yale majengo yote ambayo hayajakamilika, tunayapangia mpango mkakati maalum kama Serikali, nimesema tulikaa katika utatu, Wizara ya Afya, TAMISEMI pamoja na Kamati ya Bunge ya Bajeti kubaini maboma yote na tumeshatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote huo ndiyo mkono wa Serikali sasa, maboma yote yatabainika, lakini tunachotaka kufanya ni angalau kila Halmashauri kwa kila mwaka japo angalau tujenge kituo cha afya kimoja kilichokamilika. Lakini sambamba na hilo, jinsi gani tutafanya kuimarisha zahanati yetu, mwisho wa siku tunakwenda katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ulivyokusudia kupeleka huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge, nikwambie kwamba ni mpango wa Serikali na tunaendelea nao na hili litaendelea kufanikiwa ndani ya kipindi chetu cha bajeti ya miaka mitano hii.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri Mheshimiwa Jafo nilitaka niongezee kidogo juu ya jambo hili la huduma ya afya ya msingi kwa namna ambavyo linaulizwa mara nyingi na imekuwa concern kubwa sana ya Waheshimiwa Wabunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wakati tunajumuisha Bajeti ya Serikali juzi, ni kweli kwamba tuna vituo vya afya vichache, tangu tumepata uhuru tumeweza kujenga vituo vya afya vya Serikali takribani 470 tu. Lakini maeneo ya utawala yamekuwa yakiongezeka Wilaya zimeongezeka Halmashauri zimeongezeka, Mikoa imeongezeka na hivyo ni lazima tufanye utafiti, tufanye tathmini ya namna catchment zilivyokaa ili tuweze kuja na mpango mzuri sana ambao utajibu maswali mengi sana ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyo sasa waridhike na Waheshimiwa Wabunge watuamini tunaendelea kufanya mchakato huo wakufanya tathmini tukishirikiana na Wizara ya Afya na kama nilivyosema juzi kwamba tukiamua kwa Halmashauri 181 tulizonazo nchini, tukasema kila mwaka tujenge kituo kimoja, kwa miaka mitatu tutakuwa tumejenga vituo 543, vituo 543 ni zaidi ya vituo tulivyovijenga vya afya toka tupate uhuru ambavyo ni 470.
Kwa hiyo, nasema Waheshimiwa Wabunge hili tunalichukua pamoja na uchache wa fedha kama mnavyosema lakini kwenye mpango huo tunaokubaliana Wizara ya Afya tutakuwa pia tuna-package ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tuna-fund siyo tu kwa maana ya ujenzi lakini pia kwa maana ya vifaa tiba, pia na wataalam.
Waheshimiwa Wabunge, hivyo, niwaombe sana tuvumiliane tuende kwa style hiyo ninaamini baada ya miaka mitano mtakuwa na kitu cha kusema kwa wananchi waliowachagua.

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ruzuku katika Hospitali ya Haydom ambayo pia ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara ambayo inatumiwa na Mikoa ya Singida, Simiyu, Arusha pamoja na Jimbo la Meatu?

Supplementary Question 4

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Wilaya ya Korogwe ina Halmashauri mbili na Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina hospitali, wananchi wake asilimia 60 wanatibiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya na kusababisha msongamano mkubwa katika hospitali hiyo. Halmashauri ya Mji tuna zahanati ipo Kata ya Majengo ambayo vilevile inalaza akina mama wajawazito wanajifungulia pale.
Je, Serikali sasa kwa maana ya Wizara ya Afya hasa ikizingatiwa kwamba hatuna hospitali itakuwa tayari kutusaidia kujenga jengo la upasuaji ili kusudi wa kina mama wale wajawazito wasiende kule kwenye hospitali ya Magunga ambako kuna msongamano mkubwa?

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu zangu kama sikosei na Mama Mary Chatanda atanisahihisha, mwezi wa Machi tulikuwa pamoja kutembelea Hospitali ya Korogwe pale, lakini tulivyoenda pale nilichokishuhudia ni umati mkubwa wa watu waliojaa katika hospitali ile, sikujua kwamba umati ule ni kutokana na congestion kutoka katika hizi Halmashauri mbili.
Nimshukuru Mbunge kwa sababu siku ile tulivyoondoka nimekuta kwa mara ya kwanza mashuka yaliyowekwa katika makabati siku hiyo wametandika katika vitanda, Mbunge alinisaidia sana tukatoa maagizo mazito kuhakikisha kwamba makabati wataalamu suala la shuka ziwekwe katika vitanda siyo watu walalie vitenge vyao. Kwa hiyo Mbunge nikushukuru katika lile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wana hiki kituo cha afya naomba niseme wazi umati mkubwa tuliouona pale naomba kwa sababu bajeti ya mwaka huu tumeshaipanga, katika bajeti inayokuja naomba tuweke mkakati wa pamoja katika kikao chetu cha Baraza la Madwani. Tutenge bajeti na Ofisi ya TAMISEMI itasimamia hilo kuhakikisha tunajenga theater ili hiki kituo cha afya tukipandishe tukipandishe hifikie hadhi inayokusudiwa, mwisho wa siku ni kwamba katika hii Korogwe Mji iwe na Hospitali yao inayojitegemea kupunguza umati wa watu katika Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe.