Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Asha Abdullah Juma
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha kimaendeleo vijana wa skauti nchini?
Supplementary Question 1
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kuwanyanyua vijana hawa wa skauti walioiva kimaadili na kizalendo, kuwatengea mgao maalum wa kupata ajira zinapotokea kama vile kwa Jeshi la Wananchi na taasisi nyingine?
Mheshimwia Mwenyekiti, swali la pili: Serikali ina mpango gani wa kutenga ruzuku malalum kwa ajili ya shughuli za Skauti Tanzania?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa vijana walioiva kiuzalendo ambao wanatoka skauti, na mara nyingi tumekuwa tukiwaangalia sana kwenye suala la ajira, na ajira hizi pindi zinapotokea ziwe za Serikali na pia kwenye taasisi na vyombo vyetu vya usalama, imekuwa ni moja ya sifa ama kigezo, kama wale walioenda Mgambo na JKT kuangaliwa kama sifa ya ziada. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwaingiza kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na pia katika majukumu mengine ambayo yanatokana, au ajira zinazotoka upande wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu ruzuku; Skauti Tanzania imeanzishwa kwa mujibu wa sheria, na bahati nzuri kabisa, Skauti Mkuu Tanzania ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo, katika utaratibu wa masuala ya kuwawezesha, kama jinsi sheria ya kuwaanzisha wao inavyoeleza, ndivyo hivyo hivyo wanaweza kupata pia fedha kupitia mifuko mbalimbali ambayo inasaidia kama sehemu ya chombo ambacho ni kama Jeshi, yaani inafanana na ile ambayo ipo katika Jeshi la Mgambo. Kwa hiyo, msaada, na pia iko fedha inayotoka Serikalini na kuna fedha ambazo ni kutoka kwa wadau mbalimbali huzitoa kupitia mifuko hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazidi kuangalia kuweza kuboresha zaidi maslahi ya Skauti wetu kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi kubwa na hasa kwenye masuala ya uokoaji pale yanapotokea majanga, sherehe za kitaifa na majukumu mengine, ahsante.
Name
Juma Usonge Hamad
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chaani
Primary Question
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha kimaendeleo vijana wa skauti nchini?
Supplementary Question 2
MHE. JUMA USONGE HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa hii. Kwa kweli vijana wetu wa skauti wametapakaa takribani nchi nzima; Bara na Visiwani. Kama Mheshimiwa Waziri alivyokiri kwamba wanafanya kazi kwenye maeneo mbalimbali. Je, Serikali haioni haja sasa kutenga mfuko maalum wa kibajeti kupitia Wilaya, Mkoa na Kitaifa zaidi ili wawe na uhakika wa fedha zao kwa ajili ya kuendesha programu zao pamoja na kufanya kazi zao kiujumla? Ahsante.
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge ambalo limefanana pia na jibu langu la msingi, na hata swali alilouliza Mheshimiwa Asha kwenye suala la kibajeti, kwamba tayari wao wana sheria ambayo inaanzisha na inatoa taratibu ikiwa ni pamoja na masuala ya kifedha, lakini kwa sababu pia ni eneo ambao linaonekana pengine lina upungufu, tutauangalia na Serikali na kuweza kuona pale panapopelea tuweze kuwasaidia zaidi na kutengeneza mifumo ambayo itawasaidia kuweza kuratibu na kutekeleza majukumu yao kama ambavyo jinsi tunawatarajia, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved