Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amina Daud Hassan
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA DAUDI HASSAN aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kutenga fedha ya mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar?
Supplementary Question 1
MHE. AMINA DAUDI HASSAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Swali la kwanza; licha ya majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za hindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Zanzibar, je, haioni haja ya kujenga kuta kandokando ya bahari ili kuzuia uendelezaji wa athari za mabadiliko ya tabianchi? Mfano kama Nungwi, Jambiani, Paje na vijiji vingine vyote vyenye fukwe ya bahari? Ahsante .
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mpango kabambe na mipango mingi ya kuhakikisha kwamba, tunakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa katika maeneo ya fukwe, ama maeneo haya ya ukanda wa Bahari, hasa katika Bahari ya Hindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tumekuwa tunahamasisha jamii ambazo zinaishi humu pembezoni mwa bahari, hasa maeneo ya ufukwe, kwanza kurejesha ama kupanda mikoko ambayo ilikuwepo lakini imekatwa, lakini hatua nyingine ambayo tumeichukua kama sehemu ya mpango kabambe wa Serikali ni kuendelea kuwaambia wananchi kwamba, wasiendelee kutupa taka hatarishi, lakini vilevile kufanya shughuli za uchimbaji wa mchanga katika maeneo haya ya fukwe. Kikubwa zaidi tumekuwa tuykiwaeleza shughuli za uvuvi, lakini pia shughuli za ulimaji ama uvunaji wa mwani zisiharibu fukwe zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa suala la ujenzi wa kingo ama kuta za kuzuia maji ya bahari au maji ya chumvi yasiingie maeneo mengine, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imeshaanza ujenzi wa ukuta kwa upande wa Tanzania Bara katika Mkoa wa Mtwara katika maeneo ya Mikindani, lakini kwa upande wa Kusini Pemba katika eneo linaitwa Sepwese, tayari tumeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maeneo ya Paje, Jambiani, Bwejuu, Nungwi na maeneo mengine, cha kwanza tunaenda kufanya utafiti kujua ni aina gani ya ukuta ambao unatakiwa, lakini tumwambie Mheshimiwa tunakwenda kutafuta fedha, ili tuone namna ambavyo tunakwenda kujenga hizi kuta ambazo zita-control uingiaji wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA DAUDI HASSAN aliuliza: - Je, kuna mpango gani wa kutenga fedha ya mabadiliko ya tabianchi kusaidia wananchi wenye visima vya maji chumvi Zanzibar?
Supplementary Question 2
MHE. FATMA TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Waathirika wakuu wa suala zima la tabianchi ni wanawake na hasa wale wanawake wanaoishi maeneo ya pembezoni. Nini mkakati wa Serikali wa kuwa na program maalum kwa ajili ya hawa wanawake wa pembezoni waweze kupata mafunzo kukabiliana na hali ya tabianchi?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, tayari alichokiomba Mheshimiwa Toufiq tumeshakianza. Tumeanza na Mkoa wa Kaskazini Unguja, tayari kule viko vikundi vya akinamama vya ujasiriamali katika Jimbo la Chaani. Tumeshaanza hiyo program ya kuwapa taaluma akinamama ili waweze kujua namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Haya tumeyafanya kwa sababu, tumeona baadhi ya shughuli za uvuvi, lakini hata shughuli za ulimaji na uvunaji wa mwani, wengi wao tumegundua ni akinamama. Kwa hiyo, tumeona tuendelee kuwapa hii elimu ili waweze kuepukana na hizi athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved