Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa Shirikisho la International Federation of Cross and Crescent nchini?

Supplementary Question 1

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naishukuru Serikli kwa kuanza mchakato huu muhimu kwa nchi yetu, hata hivyo nina maswali mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mchakato huu wa kusajili Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC)tumeambiwa uko kwenye mchakato kwa kipindi kirefu sana, takribani miaka thelathini sasa. Serikali sasa inatuambia mchakato utakamilika lini na mkataba kusainiwa ili shirika hili lianze kufanya kazi hapa nchini kwetu?

Swali la pili Serikali imejipanga vipi kulinda maslahi ya Watanzania katika mikataba itakayosainiwa ili kuhakikisha shirika hili la Kimataifa litakapoanzishwa ajira kwa Watanzania zitakuwepo kuliko kuajiri watu wa nje zaidi? Ahsante. (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Judith Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze sana Red Cross Tanzania wamekuwa wakisimamia mchakato huu kwa muda mrefu sana kuweza kuhakikisha hata hatua hii inaweza kufikiwa na wamekuwa wakifanya kazi kubwa, kazi mbalimbali za Kitaifa, sherehe za Kimataifa, wakati wa maafa, pia wamekuwa wadau muhimu sana wa Serikali katika masuala ya maafa kwa hiyo ninawapongeza sana, pili ninawapongeza uongozi ambao umefanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ambalo ameeleza kuhusiana na kuchukua muda mrefu, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, tayari itifaki zote zimeshafanyika. Kwanza kuwasiliana na Shirikisho lenyewe; pili, kukutana na wadau na tatu, sasa iko kwenye hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje katika kukamilisha tu itifaki za Serikali na taratibu za ndani ili kuweza kufanikisha jambo hili. Ndiyo maana tukasema kama Serikali kwamba sasa limefikia mwisho. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa hatua za ufuatiliaji.

Mheshimiwa Spika, pili, swali lake la kuhusiana na masilahi, ni kweli kwamba mashirika haya kimataifa yamekuwa yakija kufanya kazi nchini lakini tunaangaliaje ajira za wazawa?

Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria hapa ya Mwaka 2005 inayoruhusu uratibu wa ajira za wageni. Imekuwa ni wakati wote, hata kwenye Sheria ya Usajili wa Makampuni Sura Na. 212 inaelekeza namna unaposajiliwa kama kampuni, taasisi au asasi za kiraia, sharti ni kwamba waajiriwe Watanzania. Inapotokea ameajiriwa mgeni ni pale tu ambapo aidha taaluma yake ni maalum sana, au ufahamu au knowledge aliyonayo ni adimu hapa nchini kwamba hatuwezi kumpata Mtanzania mwenye sifa hiyo. Kwa hiyo, nitoe agizo hapa kwa taasisi zote, mashirika ya Kimataifa pamoja na Makampuni ya kiuwekezaji ya nje yaendelee kuzingatia utekelezaji wa Sheria ya Mwaka 2005 ya Kuratibu Ajira za Wageni inayowataka waangalie matakwa ya ajira za Watanzania.

Mheshimiwa Spika, pia usajili wa IFRC utakuwa chini ya msukumo wa Red Cross Tanzania. Tutawaomba Red Cross nao waendelee kutusaidia kupata taarifa na kuratibu ili ajira za Watanzania zisipotee, ahsante sana.