Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nicodemas Henry Maganga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbogwe
Primary Question
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuza: - Je, kuna mpango gani wa kuongeza thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na nchi jirani za Afrika Mashariki?
Supplementary Question 1
MHE. NICODEMAS HENRY MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, anafahamu usumbufu wanaoupata wafanyabiashara kwenye mipaka yetu, kwa maana ya mipaka ya Kenya na Rwanda, kwa vile kule kila wakati faranga inapanda bei na kushuka lakini shilingi nakumbuka mwaka 1995 enzi za Mkapa ndiyo shilingi ilipanda bei na hii ndiyo inachangia ugumu wa maisha.
Sasa kuna mkakati gani wa kuifanya shilingi yetu iwe na thamani ili wananchi waweze kupata bidhaa kwa bei nafuu kulingana na upandishaji wa thamani?
Swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mfumuko wa dola, kwa sababu kumekuwa na kupanda sana kwa dola bila utaratibu. Leo unakuta dola inabadilishwa kwa shilingi 2,550 lakini jioni ukienda tena unakuta inabadilishwa kwa shilingi 2,800 na hii inafanya Taifa kuwa na maisha magumu, ahsante sana. (Makofi)
Name
Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Answer
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza. Moja, Serikali imejitahidi kusimamia kuhakikisha la kwanza, thamani ya shilingi haishuki; la pili, ambalo tunalifanya katika mikakati yote hii ambayo unaiona Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu aliyoielekeza ya kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji, malengo ya muda mrefu kwenye hilo ni kwenda kuimarisha, kuongeza thamani ya shilingi yetu. Tutaongeza thamani ya shilingi yetu kwa namna nyingi zikiwemo hizo mbili za kuongeza mauzo nje ili tuwe na dola nyingi. Pili, kwa kuzalisha bidhaa ambazo tunaweza tukajitegemea na tukatumia ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kudhibiti mabadiliko ya haraka haraka ya bei ya dola, Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi cha muda mfupi, tunalishughulikia jambo hili ili kuweza kukabiliana na tatizo ambalo limejitokeza la dunia nzima la upungufu wa dola, ambapo hicho ndicho kinachosababisha mahitaji ya dola yanakuwa makubwa kuliko upatikanaji wa dola na hivyo kufanya bei ya dola kuanza kubadilikabadilika.
Mheshimiwa Spika, hata sasa tuna hatua ambazo tumeendelea kuzichukua ambazo tunaamini zitaweza kusaidia dola ziwepo nyingi sokoni, na zikiwa nyingi sokoni zitasababisha tatizo la bei kubadilikabadilika kuweza kupungua.
Mheshimiwa Spika, tunatoa rai kwa wadau wote wanaoshiriki katika soko la kubadilisha fedha, waendelee kushiriki kikamilifu ili kuweza kuhakikisha kuwa Dola haiadimiki sokoni na hivyo kusababisha bei kubadilikabadilika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved