Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Josephat Mathias Gwajima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Primary Question
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kuitumia Bahari kwa michezo mbalimbali ya majini ili kuongeza kipato cha wananchi wa Jimbo la Kawe?
Supplementary Question 1
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nusu ya Jimbo la Kawe kwa maana ya Msasani, Masaki, Oysterbay, Kunduchi, Mbweni, Kawe, Bunju, Sea Cliff na Coco yote iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuendeleza hii michezo ya Bahari kwa ajili ya afya, burudani na kipato cha watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, je, utakubali Jumapili hii tuandamane pamoja tukafungue Ligi ya Rede kwa michezo inofanyika katika Jimbo la Kawe? (Kicheko/Makofi)
Name
Hamis Mohamed Mwinjuma
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Answer
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuchukua nafasi hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Josephat Gwajima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kwa kuona fursa kubwa iliyopo katika mchezo wa soka la ufukweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, soka la ufukweni katika nchi hii limeanzishwa rasmi mwaka 2014 na ni kwa miaka tisa tu ambayo tumekuwa tukilifanya, lakini limeonyesha kuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa tuko Namba Tano kwa Bara la Afrika kwa soka la ufukweni na Namba 42 kwenye rank za FIFA za kidunia kwa soka la ufukweni, namba ambazo hili soka letu la kawaida hatujawahi kuzifikia na pengine itatuchukua muda mrefu kidogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na TFF kwa kushirikiana na Serikali, kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye michezo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wanao mpango mkakati wa miaka mitano, ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha kwamba soka la ufukweni linafundishwa mashuleni na vyuoni na kila Mkoa ambao una fukwe kuweza kuwa na ligi yake kwa ajili ya soka la ufukweni. Lengo ni katika kipindi cha miaka mitano hii inayofuata tuwe na wachezaji angalau 10,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeanzisha mazungumzo na JKT na wadau wengine kadhaa ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji kwa ajili ya soka la ufukweni. Pia, kumekuwa na mashindano ya Copa Dar es Salaam ambayo yanazishirikisha nchi mbalimbali kama Burundi, Uganda, Comoro, Ushelisheli na Malawi, mwaka huu tuna mpango wa kuwaalika Kenya, Oman, Morocco na Senegal. Kwa hiyo, tutakuwa na Ligi ya Soka la Ufukweni yenye nchi Tisa, ambapo ni wazi kabisa itaongeza Pato la Taifa lakini wachezaji wetu wengi watashiriki na itatoa ajira za moja kwa moja na ajira nyingi nyingine zinazozunguka mchezo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, najua Askofu utakuwa na maono, umengundua kama Jumapili ninao muda na tutaambatana mimi na wewe kwa ajili ya kwenda kuanzisha Ligi yako ya rede pale Jimboni Kawe. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved