Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Catherine Valentine Magige
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: - Je, upi mpango wa kudhibiti wanyama wanaoharibu mazao na kugharimu maisha ya watu Kata za Naarami, Lokisale, Moita, Lepruko na Makuyuni?
Supplementary Question 1
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spikja, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni nimefanya ziara Wilayani Monduli na moja kwa moja Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alizungumza na wananchi wa Monduli, akawaahidi baada ya wiki moja ya ziara yangu ataenda na wataalam wake kutatua kero hii, lakini mpaka leo hii Waziri hajaonekana. Matokeo yake mwezi uliopita mwananchi mmoja katika Kata ya Makuyuni eneo la Ndoroboni ameuawa na tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tatizo la tembo limekuwa kero kubwa sana kwa Tanzania nzima, wamekuwa wanazagaa zagaa ovyo na kuharibu mazao na kuua wananchi, Serikali imekuwa inatupa majibu hatuoni matokeo yake. Sasa leo nataka kufahamu nini kauli ya Serikali? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kumekuwa na tatizo hili la changamoto la wanyama wakali na waharibifu, ni changamoto sasa takribani miaka minne inaendelea kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua za haraka. Moja ya hatua za haraka ni kwamba tumeanza sasa hivi kuwarudisha hawa wanyama wakali kwa kutumia helikopta, kuna baadhi ya maeneo tayari tulishaanza kwenda. Wakati huo huo tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa sababu ukiangalia maafa kwa asilimia kubwa yanajitokeza ni pale wananchi hawana elimu, wengine wanafukuza kwa kutumia fimbo na kadhalika. Kwa hiyo tunaendelea kuitatua hii changamoto wakati huo huo na kutoa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ya haraka ni kwamba sasa hivi tumeamua tutapeleka Askari ambao watakaa katika maeneo husika kwa muda mrefu. Suala la kupigia simu Askari ndiyo wafike sasa hivi tunataka kuliacha na tunataka hawa Askari kwenye maeneo yale hatarishi wakae maeneo yale wakishirikiana na wale VGS (Village Scouts) ili kuondoa hili tatizo kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna operesheni ambayo tumeipanga na Mheshimiwa Waziri ameelekeza na tayari tutaingia kazini mara moja. Kwa hiyo, naomba niwatoe wasiwasi wananchi kwamba Serikali inalishughulikia suala hili kwa karibu sana na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, umetuelekeza tulishughulikie kwa uharaka, tunatambua wananchi wanaumia lakini naomba nitoe kauli hii kwamba wananchi tutawafikia muda siyo mrefu. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved