Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Nancy Hassan Nyalusi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:- Je, lini Serikali itaboresha mafao ya Wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata Mstaafu kwa mwezi?
Supplementary Question 1
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha kwamba, inaondoa usumbufu kwa wanachama kupata mafao yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, kwa nini Serikali imeamua kuunganisha Mifuko ya Pensheni, haioni kwamba, imechangia kuzaa changamoto? (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA. VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nancy, kama alivyouliza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wetu wa Hifadhi ya Jamii au Mifuko yote kwa pamoja PSSF na NSSF imeweza kwa sehemu kubwa sana kuondoa changamoto za ulipaji wa mafao kwa wakati. Kwa kufikia sasa tunalipa ndani ya siku 60 kama mfanyakazi atakuwa hana changamoto zozote za kitaarifa au kumbukumbu na hata wakati mwingine tunalipa hata chini ya siku saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ambazo Serikali imechukua kupunguza usumbufu ni pamoja na kuweka Mfumo wa TEHAMA ambapo mwanachama anapata taarifa zake kupitia simu yake ya kiganjani na hatua nyingine mojawapo, pia ilikuwa ni hii ya kuunganisha Mifuko ili kuweza kutengeneza utaratibu wa uwiano katika malipo, lakini pia ulinganifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, lilikuwa ni katika kutoa usumbufu, kwa nini Mifuko iliunganishwa. Mifuko hii iliunganishwa, la kwanza kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya uwiano wa mafao. Mtu alikuwa PPF na aliyekuwa LAPF unakuta wote wamefanya kazi sawa na wamestaafu sawa na wametumikia Taifa sawa, lakini mmoja unaweza ukakuta katika pensheni yake mwishoni akalipwa milioni 40 na mwingine milioni 75 kwa sababu ya utofauti wa Mifuko, lakini kwa hiyo, kutengeneza ulinganifu wa mafao tukaona ni bora kuweza kuunganisha Mifuko hii baada ya kupata utafiti uliofanywa kama actuarial evaluation.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili, ilikuwa ni uendelevu wa Mifuko. Uendelevu wa Mifuko hii kwa sababu ya kuwa mingi ilikuwa inasuasua sana katika kujisimamia na kuwa na uendelevu wake. Mpaka sasa baada ya kuchukua hatua ya kuiunganisha thamani iliyokuwepo kwa PSSF ilikuwa ni trilioni tano, lakini sasa Mfuko umeweza kufika zaidi ya trilioni 8.1. Kwa hiyo, unaweza ukaona tofauti hiyo kubwa kama faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ilikuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji. Hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa zaidi ya mitano, sasa unakuta yote ina Menejimenti, Bodi na huku kuna Menejimenti, lakini pia kuna Bodi, kuziendesha na kulipa mishahara, gharama za operational cost na kadhalika zote zilikuwa kubwa sana. Tumeweza kufanikiwa kwa Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupunguza hasara hiyo ya gharama ya uendeshaji kutoka asilimia 12 mpaka asilimia tano.
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:- Je, lini Serikali itaboresha mafao ya Wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata Mstaafu kwa mwezi?
Supplementary Question 2
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Imekuwa vyema ambavyo mifuko hii inawekeza na kuwa na majengo ya kibiashara, lakini mfanyakazi ananufaikaje na biashara hizo? Pia tunajuaje wamepata kiasi gani na mwananchi wa kawaida anapokwenda kustaafu anapataje gawio sahihi katika Mifuko hiyo ambayo wamewekeza?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA. VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda. Ni kweli kwa kuangalia tija ya wanufaika wa Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii. Kile kinachochangiwa na mwanachama ukikipigia hesabu hata mwanachama yeyote kokote aliko akipiga hesabu ya fedha ambayo ameichangia mpaka kustaafu kwake na kile ambacho anaenda kukipata kama malipo ya mkupuo na kile anacholipwa mwisho wa mwezi ni kikubwa kuliko kile ambacho alichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale waliokuwa katika Mifuko mingine unakumbuka PSPF wakati huo, lakini pia LAPF na NSSF fedha yake thamani imeongezeka ambayo ni ongezo kama faida ya uwekezaji na ulindaji wa thamani ya fedha kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 67. Hii ni hatua kubwa sana ambayo Serikali imefanya na hata wenzetu nchi jirani, sitaitaja lakini, wamekuja kuiga mfano wa namna gani ambavyo tumekuwa tukiongeza maslahi ya wastaafu kutokana na uwekezaji unaofanyika katika mifuko, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved