Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ng'wasi Damas Kamani
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:- Je, Serikali inatumia mfumo gani kuhakiki ubora na matokeo chanya ya programu mbalimbali zinazotolewa kwa vijana?
Supplementary Question 1
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa lengo kuu la hizi programu ni kutatua changamoto kubwa za vijana ikiwemo kukuza elimu ya ujuzi na kutatua changamoto ya ajira, kumekuwa na changamoto ya vijana wengi ambao wananufaika na hizi programu kushindwa kuunganishwa moja kwa moja na masoko ya ajira na mitaji pale wanapohitimu. Sasa, ni upi utaratibu au mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapohitimu programu hizi wanaunganishwa moja kwa moja na masoko ya ajira au mitaji ili wasirudi mitaani na kuondoa tija ya hizi programu wanazopata?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, bado kuna changamoto ya taarifa hasa kwa vijana wengi waliopo vijijini ya namna gani programu hizi zinapatikana, vigezo na utaratibu wa kuweza kupata programu hizi. Sasa ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaboresha mifumo ya taarifa ili vijana wengi wa Tanzania waweze kufahamu fursa hizi na kunufaika nazo?
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu ambao Serikali inaendelea nao na tumekuwa tukiendelea kuufuatilia na kufanyia tathimini kuhusu namna ya kuunganishwa na ajira lakini pia kupata fursa za mitaji. Wote tutakuwa mashahidi kuwa kupitia Halmashauri zetu wapo Maafisa Maendeleo ya Vijana lakini pia Maafisa Maendeleo ya jamii. Wote hawa wanaendelea kutoa mafunzo kwa utaratibu wa mwongozo. Mikopo ya asilimia kumi kwanza inatangazwa lakini pili ni takwa la Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tatu inaendelea kutangazwa katika Halmashauri zetu zote. Viongozi wengi sana na hata Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakihamasisha uwepo wa ile mikopo ya asilimia kumi. Pia ipo mifuko mingine ya uwezeshaji vijana ukiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao upo Ofisi ya Waziri Mkuu na tumekuwa tunautangaza kupitia Mwenge wa Uhuru.
Mheshimiwa Spika, pia zipo programu nyingine katika wizara za kisekta. Ipo mipango ya kisekta ya kuwasaidia vijana kwa mfano kwenye masuala ya fursa za ajira, kuwaandaa kwenye ajira na mitaji. Pia tuna Wakala wa Ajira (TaESA) ambaye ana jukumu kubwa; kwanza la kuwatambua vijana wote wahitimu, pili kuwapeleka kwenye programu mbalimbali ikiwepo utarajali na kuwapeleka kwenye mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Wizara zote za Kisekta zimekuwa na programu za vijana zinazohusiana na uandaaji wao wa kupata ajira hata ukiangalia Wizara ya Kilimo tunayo Building a Better Tommorow (BBT) ambayo ni kwa ajili ya kilimo biashara. Wizara ya Mifugo na Uvuvi nayo ina programu ambayo ni BBT Life ambayo inahusiana na unenepeshaji mifugo.
Mheshimiwa Spika, hao wote wamekuwa wakikutanishwa na masoko ya ajira lakini pia masoko ya malighafi ambazo wanazitengeneza katika maeneo hayo. Nikiongelea la mwisho ambalo ameniuliza kuhusu changamoto za vigezo na taarifa, hili limeelezwa wazi kwenye mwongozo wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi yaani 4:4:2, almaarufu katika Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, hata sisi kwa upande wa Wizara tumeendelea kufanya hivyo siyo tu katika ufuatiliaji na tathimini lakini pia tumeendelea kutoa elimu kwa vijana na kuitangaza katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, ahsante.
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:- Je, Serikali inatumia mfumo gani kuhakiki ubora na matokeo chanya ya programu mbalimbali zinazotolewa kwa vijana?
Supplementary Question 2
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko miongoni mwa baadhi ya vijana kwamba hizi programu za mendeleo kwa vijana na hasa zile za kwenda nje zinavyotolewa kunakuwa na upendeleo. Sijui Serikali inasemaje kuhusu tatizo hilo ambalo linalalamikiwa sana? Ahsante.
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakuhakikishia kwamba Serikali hii haina upendeleo kabisa. Serikali ya Awamu ya Sita imeweka wazi vigezo vya vijana kuweza kupata fursa hizi. Tumekuwa tukizitangaza kwenye vyombo vya habari, tumekuwa pia tukiwaambia Waheshimiwa Wabunge fursa zilizopo. Kuhusu fursa za kwenda nje, tumeingia katika billeteral agreement, na mikataba ya kuhusiana na namna gani vijana wanaweza kupata fursa za ajira tulishaieleza.
Mheshimiwa Spika, wapo Mawakala wa Ajira za nje ya nchi ambao wamesajiliwa chini ya Ofisi ya Kamishna wa Kazi. Pia kupitia TaESA pamoja na SUGECO tumekuwa tukitafuta wahitimu wanaofanya vizuri kwenye vyuo vyote vikuu ikiwemo Chuo cha Kilimo (SUA). Wanafunzi ambao wanafanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali wanapata fursa za kwenda kufanya masomo nje ya nchi kwa mfano nchini Israel. Sasa hivi wataenda vijana takriban 600 katika programu hizo.
Mheshimiwa Spika, tunachagua vijana ambao wamefanya vizuri na reccomendation hii inafanywa kwa usaili kwa kupitia Chuo Kikuu chenyewe na kuangalia yale matokeo ya nani amefanya vizuri. Kwa hiyo, hakuna Mtanzania ambaye anazuiwa kufanya vizuri na yeyote anayefanya vizuri anachukuliwa na Serikali kwa ajili ya kwenda kupata masomo hayo nje ikiwa ni sambamba na kupata fursa mbalimbali kulingana na sifa na vigezo ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa sheria bila upendeleo, ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved