Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Anna Richard Lupembe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Primary Question
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa lambo Kata ya Nsimbo, Kijiji cha Mwenge, Halmashauri ya Nsimbo?
Supplementary Question 1
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya ucheleweshwaji wa mradi huu masika ikakuta mradi umecheleweshwa na mvua za masika, lakini Mkandarasi alichukua muda mrefu sana kuingia site katika kujenga mradi huu na mradi huu unajengwa na Wizara, haushirikishi Halmashauri ambayo wako katika eneo husika la mradi.
Je, Serikali ina mkakati gani kushirikisha kwa ukamilifu Halmashauri ya Nsimbo ili kuendelea kusimamia mradi huu?
Swali la pili, Serikali inachelewesha malipo ya Mkandarasi, Mkandarasi anashindwa kutekeleza mradi kutokana na kukosa kulipwa pesa. Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi pesa zake ili aweze kukamilisha mradi? (Makofi)
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza miradi hii ni miradi ya Serikali, haijalishi mradi unatekelezwa na Wizara ama unatekelezwa na Halmashauri, miradi hii yote ni ya Serikali. Miradi hii inapokuja huku kwenye Halmashauri maana yake mamlaka zote za Serikali zinapaswa kushiriki katika kutekeleza mradi huo, kwa sababu miradi hii haimaanishi kwamba inapojengwa na Wizara ni kwamba Serikali nyingine haihusiki, Hapana! Sasa hii ni dhana ya uelewa katika Halmashauri zetu kwamba miradi inapokuja kwa namna moja au nyingine ni lazima watumishi wa Halmashauri washiriki kwa namna moja ama nyingine katika kusimamia mradi huo ili kuleta tija na ubora wa miradi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua namna ya ucheleweshaji wa malipo. Malipo ya Serikali yoyote yanalipwa kulingana na certificate ya utekelezaji wa mradi alipofikia huyo Mkandarasi. Serikali inalipa fedha kutokana na certificate alizo-raise ambazo zinatokana na kazi aliyoifanya kwa kiwango hicho na huyu mkandarasi mpaka sasa ameshalipwa zaidi ya asilimia 70 ya malipo yake kwa sababu jumla ya shilingi milioni zaidi ya 270 amekwishalipwa kati ya milioni 510.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mkandarasi huyu anakwenda vizuri na ukiona mradi unachelewa ni kwa sababu ya upatikanaj wa fedha lakini ni pamoja na kwamba kazi anayoifanya ndiyo itakayo-determine analipwa fedha kiasi gani, kwa hiyo, huyu analipwa kulingana na kazi anayoifanya. Naomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved