Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUILINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, lini Serikali itatoa fidia kwa Madaktari na Manesi wanaopoteza maisha wakihudumia Wagonjwa wa Magonjwa ya Mlipuko?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itafanya mapitio upya ya Sheria Na. 263 ya Mwaka 2015 ili kuongeza fidia na pensheni kwa watumishi hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili ni kubwa ambalo linapelekea kwamba Madaktari na Manesi pindi inapotokea magonjwa ya mlipuko wanakosa ari na moyo wa kufanya kazi kutokana na fidia ndogo ambayo wanaipata. Je, Serikali imefanya utafiti wa kina juu ya tatizo kubwa namna hii? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake amabalo kwa kweli linalenga kuboresha huduma lakini kuwatia ari watumishi wa afya. Kwanza, ameuliza kwamba ni lini Serikali itakaa na kujadili ni namna gani tunaweza kuboresha hili. Hili suala linahitaji siyo Wizara ya Afya peke yake linahitaji Wizara mbalimbali za sekta husika kulingana na tatizo lilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe Wabunge kwa sababu mmelisema hili hapa, basi tutaenda kufanya mawasiliano na kukaa na wenzetu na Serikali ikitokea mjadala ndani ya Serikali ikionekana kuna uhitaji huo basi italetwa hapa Bungeni kwa ajili ya kubadilisha, lakini turuhusu kwanza likatazamwe na wataalam ili tuone linaweza kufanywajwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba watumishi wengi wanaogopa kufanya kazi kwenye maeneo yao, kwa sababu wanaogopa kupata matatizo. Mimi nikwambie tu kwanza nitumie fursa hii kuwapongeza watumishi wa afya Tanzania, tulipata tatizo Kagera watumishi wetu hawakutazama kuna hatari gani wakati watu wengine wanakimbia kwenye majanga wao walikimbilia kwenye eneo la tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania Waziri wetu wa Afya alikwenda Marekani juzi kwenye Umoja wa Mataifa walimpongeza kwa kushangaa ni kwa namna gani ndani ya siku 78 Tanzania imeweza ku-control Marburg. Maana yake hizi ni juhudi za watumishi wetu hawa ambao wana moyo, wana nia njema ya kuwahudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnajua wakati wa corona kila mtu alikuwa anakimbia, kila mtu anaogopa kwenda hospitalini lakini watumishi wetu walikimbia na wakafanya na umeona kilichotokea Tanzania na vifo vingi havikuwepo Tanzania kama maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hawa watumishi kwa kweli pamoja na mazingira mengine na matatizo mengine, wanafanya kazi nzuri sana na wana moyo mzuri. Kwa hiyo, nikuambie tu hawaogopi lakini kwa ukweli halisi hebu tukayaangalie haya mengine ambayo umeyasema hapa yaonekane kama kuna sababu ya kufanya hivyo tuende nayo na kuboresha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akimuelekeza Waziri wetu. Kwa mfano, kuna kijana aliyepata shida kule Kagera na Mheshimiwa Rais wetu alielekeza na yule kijana alipewa zaidi ya Shilingi Milioni Kumi, kama incentive tu kupitia masemo wa Mheshimiwa Rais wetu na sasa hivi amaepewa shilingi 10,000,000 yake na anaendelea na shughuli zingine za Kisheria na haki zake za Kisheria bado anaendelea kuzipata. Kwa hiyo, tutaendelea kuwatia moyo kwa namna hiyo, lakini nikuambie tu kwamba Watumishi wana ari sana. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwanza kumshuruku Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maelezo mazuri, pia nimesimama kumshukuru Mheshimiwa Jacqueline Msongozi kwa swali lake. Nimesimama kwa sababu kipaumbele cha kwanza cha Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupambana na magonjwa hatarishi na magonjwa ya mlipuko ni kuwalinda watumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatufanyi kitu chochote. Kwanza tunatoa training kwa watumishi wa afya jinsi gani ya kuhudumia wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko. Pili, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatuwezesha kutoa vifaa kinga vya kutosha kwa ajili ya watumishi wa afya, lakini pale kutakapotokea changamoto amesema vizuri Naibu Waziri Serikali inafanya kila linalowezekana kuokoa maisha ya mtumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Kagera tulikuwa na mtumishi Daktari mmoja alipata maambukizi ya Marburg kwa sababu ya kumhudumia mgonjwa, tulipeleka dialysis mashine Kagera, tumepeleka Madaktari Bingwa Saba na Wauguzi Bingwa na leo Daktari yule tumeweza kuokoa maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimesimama kwanza kuwashukuru watumishi wa afya. Watumishi wetu wa afya siyo waoga, hawajawahi kukimbia wagonjwa. Pili, nimesimama kuwahakikishia Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia itatoa kipaumbele cha kuwalinda watumishi wa afya katika kupambana na magonjwa ya mlipuko na magonjwa hatarishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama ili kuweza kuwatia moyo watumishi wa afya, hatujawahi kuona Watumishi wa Afya wamekimbia wagonjwa Tanzania.