Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. AMEIR A. AMEIR aliuliza: - Je, ni asilimia ngapi ya Wafanyabiashara hawajaingizwa katika Mfumo rasmi wa kodi na Serikali inachukua hatua gani kuwafikia?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna idadi ndogo sana ya usajili kwa maana ni asilimia 16 tu ya nguvu kazi ya walipa kodi: Je, Serikali haioni wakati umefika sasa kwa Wizara ya Fedha, TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa pamoja na kuona namna bora ya kusajili wafanyabiashara na walipa kodi katika ngazi ya vijiji badala ya kugombania leseni kwa maana ya leseni B?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ya kimkakati, mfano Jimbo la Mikumi ambalo siyo wilaya wala siyo halmashauri, lakini ni maeneo ya kimkakati ya biashara na kodi: Serikali ina mpango gani wa kuchechemua maeneo haya ili wafanyabiashara washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli kama nilivyosema, bado idadi ya walipa kodi ni ndogo na tayari Serikali ina mikakati mbalimbali ili kuhakikisha tunaongeza idadi ya walipa kodi kulingana na nguvu kazi iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Ufanyaji Biashara nchini (MKUMBI), na hili tumeendelea kutoa elimu na hatua mbalimbali ambazo zinapelekea kuvutia wafanyabiashara na wazalishaji mbalimbali kurasimisha biashara zao ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi, tozo na ada ambazo ni kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeendelea kuweka mazingira ambayo yanarahisisha usajili wa biashara kwa wananchi wote. Kwa hiyo, tayari Serikali inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, TAMISEMI lakini pia Wizara ya Viwanda. Sasa hivi tunataka tuone namna ya kuhakikisha tunapeleka maelekezo kwenye ngazi ya vijiji ili kuwa na dirisha la pamoja la kuratibu masuala ya biashara kutoka ngazi ya Kijiji, lakini tayari tumeshafika kwenye halmashauri ambako tunaweka Idara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji ambao watafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, maeneo mkakati, ni kweli tunaona umuhimu wa kuhakikisha maeneo ya kimkakati ambayo yana fursa nyingi za kibiashara kuyawekea miundombinu wezeshi ikiwemo masoko na kuweka vituo maalum vya kuhamasisha wananchi kusajili biashara zao. Tayari Wizara kupitia BRELA tumeshaanza kupeleka elimu na kuhamasisha wananchi kusajili biashara zao katika maeneo husika kwa maana ya halmashauri na hata katika maeneo yale ya kimkakati ambayo tunaona yana biashara ambazo zinaweza kuleta tija kwa uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.