Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Michael Mwita Kembaki
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Mjini
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa majibu mazuri lakini napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini Serikali itapeleka fedha kukamilisha ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari ya Mogabiri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Shule ya Sekondari Tarime mabweni yana uwezo wa ku-accommodate watoto 750 lakini wanafunzi waliopo katika shule ile ni zaidi ya 1,500. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni zaidi ili kutoa huduma ya mabweni mazuri katika Shule ya Sekondari Tarime?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kembaki. La kwanza kuhusu mabweni katika Shule ya Sekondari Mogabiri kwamba ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa mabweni.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba Serikali Kuu ilipeleka shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na madarasa mawili katika shule hii. Walibadilisha eneo ambalo lilikuwa limewekwa mwanzo kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya hivyo kupelekea gharama za ujenzi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, tathmini imeshafanyika na Halmashauri ya Tarime Mji na imefahamika kwamba inahitajika shilingi milioni 120 kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni haya. Serikali iko katika mchakato wa kutafuta fedha hizi kupitia mapato ya ndani ya halmashauri yenyewe na Serikali Kuu ili kuweza kumalizia ujenzi wa mabweni haya. Mkurugenzi wa Halmashauri hii tayari ameshaleta maombi hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la Shule ya Sekondari ya Tarime kuwa na wanafunzi wengi, ni kweli kwamba shule hii ina wanafunzi wengi. Kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kupanga wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu shule hii ilipelekewa wanafunzi wachache kulingana na miundombinu ambayo ipo. Tunaendelea kutafuta fedha ili kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukapeleka kwa ajili ya kuongeza mabweni katika shule hii ya Tarime Sekondari.
Name
Aysharose Ndogholi Mattembe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 2
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Masinda, Kata ya Ihanja, Jimbo la Ikungi Magharibi hutembea umbali mrefu kufuata huduma za masomo. Napenda kujua je, ni lini Serikali itajenga bweni katika shule hiyo ili kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga mabweni katika Kata hizi za Msinda na Ihanja ambazo wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufuata elimu kadri ya upatikanaji wa fedha. Natoa wito kwa halmashauri hii waanze kujenga kwa mapato yao ya ndani wakati Serikali Kuu inatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kumalizia majengo haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka shilingi bilioni tatu katika Mkoa wa Singida kwa ajili ya ujenzi wa shule ya wasichana pale Solya. Ambayo watoto wote wa kike katika Mkoa wa Singida wataenda pale Solya kwa ajili ya kupata elimu ambapo tayari kuna mabweni. Hivi karibuni kuna shilingi bilioni moja nyingine imeongezwa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ile ya Mkoa wa Solya.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ya kwanza umesema imepeleka kiasi gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali ilipeleka shilingi bilioni tatu na sasa imepeleka shilingi bilioni moja.
SPIKA: Sawa, maana ulisema shilingi milioni tatu sasa nataka Taarifa zetu Rasmi za Bunge zikae sawa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni shilingi bilioni tatu.
Name
Dr. Florence George Samizi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi.
Je, ni lini Serikali itajenga bweni katika shule ya sekondari ya Busagara ili tuweze kutoa huduma ya Kidato cha Tano na cha Sita kama tulivyoomba?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga mabweni katika shule hii ya Busagara kadri ya upatikanaji wa fedha. Mkurugenzi wa Halmashauri aanze kutenga fedha kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya na kisha kuleta maombi Serikali Kuu kwa ajili ya kumalizia mabweni haya ambayo yataanza kwa jitihada za halmashauri yenyewe.
Name
Mwantumu Mzamili Zodo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 4
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali imepeleka shilingi milioni 470 kwa shule za Kata 231. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha za mabweni kwa ajili ya shule hizo? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 470 zilizopelekwa kwenye shule hizi 231 nchini ilikuwa ni kwa ajili ya kata ambazo hazina sekondari bado katika Taifa letu hili la Tanzania. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliona kuna umuhimu wa kuhakikisha kata ambazo bado hazikuwa na sekondari zinapata sekondari na ndiyo maana ametoa shilingi milioni 470 na mwaka huu kuna shilingi milioni 560 na kuna wengine wamepata hadi shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa shule hizi za Kata.
Mheshimiwa Spika, tutakapomaliza ujenzi wa shule hizi za kata Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya mabweni kwenye shule hizi.
Name
Salome Wycliffe Makamba
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 5
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Serikali itapeleka lini fedha za kumalizia ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari ya mfano ya wasichana ambayo ipo katika Jimbo la Shinyanga Mjini?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali kwanza inamalizia miundombinu mingine, hii ni shule kama niliyosema mwanzo ya Singida ya shilingi bilioni tatu ambayo imejengwa pale Shinyanga Mjini.
Mheshimiwa Spika, Shinyanga Mjini walipata bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule hii ya wasichana ya Mkoa wa Shinyanga, na tayari kuna shilingi bilioni moja nyingine Serikali hii ya Awamu ya Sita imepeleka kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu iliyokuwa imesalia na baada ya hapo itafanyika tathmini nchi nzima kwa ajili ya mabwalo ambayo yanakuwa bado hayajakamilika ili Serikali iweze kutafuta fedha na kuipeleka kwenye ukamilishaji huo.
Name
Subira Khamis Mgalu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 6
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hizi shilingi milioni 470 kuna baadhi ya maeneo sekondari hizi hazikukamilika bado maabara nyingine hazikukamilika, je, Serikali ina mpango gani wa kufanya tathmini ya kina na kuweza kuongeza ili miundombinu ya shule hizi mpya ikamilike? Ahsante sana.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Subira Mgalu. Hizi shilingi milioni 470 ambazo zilikwenda kwenye ujenzi wa shule za Kata kwenye kata ambazo hazikuwa na shule zilienda na maelekezo maalum na zilitakiwa kutosha. Kuna Halmashauri kwa mfano pale Kongwa Mkoani Dodoma na Bahi Mkoani Dodoma walimaliza kwa shilingi milioni 470. Ni wao kule chini ambao hawakutekeleza maelekezo yaliyopelekwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wakategemea kuna fedha nyingine ya kuja kumalizia.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishafanya tahmini na baada ya tathmini hiyo ikaongeza fedha kwenye awamu hii ya pili kutoka shilingi milioni 470 mpaka kwenye minimum ya shilingi milioni 560 katika halmashauri zote hapa nchini. Tutaendelea na tathmini kuona ni namna gani tunaweza tukatafuta fedha kwa ajili ya kumalizia kule ambapo hawakumalizia lakini wengine ilikuwa ni uzembe wao wenyewe.
Name
Constantine John Kanyasu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 7
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa fedha hizi shilingi milioni 470 ziligawanywa kwa kiwango sawa nchi nzima wakati gharama za ujenzi hazifanani kati ya Dar es Salaam na mikoa mingine, ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba wanapogawa fedha zisifananishwe katika mikoa yote? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama nilivyokuwa nimemjibu Mheshimiwa Subira Mgalu namjibu Mheshimiwa Kanyasu. Baada ya shilingi milioni 470 hii kwenda na kuonekana kuna changamoto baadhi ya maeneo kwa mfano Makete kwa Mheshimiwa Festo Tuntemeke Sanga, wao mchanga wanauchukua Makambako kuweza kwenda kujenga kule Makete kwa hiyo, gharama inakuwa tofauti.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kwenye awamu hii ya pili fedha ikaongezwa kwa kulingana na maeneo. Fedha waliyopata Dar es Salaam siyo aliyopata Mheshimiwa Sanga kule Makete na siyo aliyoipata Mheshimiwa kule Mbinga Vijijini.
Name
George Natany Malima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 8
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Shule ya Sekondari ya Berege yenye Kidato cha Tano na cha Sita ina idadi kubwa ya wanafunzi lakini ina upungufu mkubwa wa mabweni. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni katika shule hii? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga mabweni katika Shule ya Sekondari Berege kule Wilayani Mpwapwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Nitoe wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuanza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya katika Shule ya Sekondari Berege na kisha kuleta maombi vilevile Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuweza kutafutiwa fedha ya kuweza kuendelea na ujenzi wa mabweni hayo.
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga Shule ya Bweni ya Wasichana Tarime Mjini?
Supplementary Question 9
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ujenzi wa hostel unahitaji miundombinu ya maji na shule nyingi hazina maji, kwa mfano Shule ya Ndugu iliyopo Mbozi. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye shule zote za hostel? Ahsante. (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni mkakati wa Serikali kuhakikisha shule zote zinazojengwa ambazo ni za bweni zinakuwa na maji. Ndiyo maana tunasisitiza coordination kati ya taasisi zote za Serikali katika maeneo husika. Pale ambapo shule inajengwa, Mkurugenzi wa Halmashauri afanye kazi kwa karibu na wenzetu wa RUWASA kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya maji inafika karibu.
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya alikotaja Mheshimiwa Neema Mwandabila kuhakikisha kwamba anawasiliana na wenzetu wa RUWASA kuvuta maji katika shule hii ambayo maji bado hayajafika.