Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Salma Mohamed Mwassa
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:- Kumekuwa na Migogoro mingi ya ardhi mjini na vijijini inayotokana na kutopima na kupanga matumizi bora ya ardhi:- (a) Je, Serikali imejipangaje kupunguza au kumaliza migogoro ya ardhi? (b) Je, lini Serikali itaandaa mipango Kabambe (Master plans) mijini na vijijini lili kuainisha matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi nchini?
Supplementary Question 1
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kuna migogoro ambayo hasa inatokana na tatizo la usimamizi mbovu wa sera. Kwa mfano, kuna matatizo yanayotokana na hawa Viongozi wa Serikali za Mitaa kuuza maeneo ya umma kama shule, zahanati, majeshi na hiyo inatokana na kwamba Serikali haijaweka zile demarcation au kutoa hati miliki katika maeneo hayo, kwa hiyo, hicho ni chanzo cha migogoro. Je, ni lini Serikali itapima haya maeneo ya umma ili kuondoa migogoro hii hasa kwa Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, fidia ni tatizo pia, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wanaanzisha Mfuko wa Fidia. Kuanzisha Mfuko wa Fidia tu sio suluhu ya mgogoro. Mgogoro wa fidia unatokana hasa na yule mlipaji kutokuwa na hela stahiki wakati anafanya uthamini. Je, ni lini sasa Serikali itasimamia kabla ya schedule ya kwenda kuthaminiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali yule mlipaji wa fidia awe tayari ameshaweka hizo hela kwenye Mfuko wa Fidia? Ahsante.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameulizia suala la tatizo la watu kuvamia maeneo ya Taasisi. Hata kabla ya upimaji ambao unatakiwa kufanyika kwa nchi nzima, Wizara ilishaelekeza kwa halmashauri zote kuhakikisha kwamba, maeneo yote ya umma yaweze kupimwa na hii inafanyika katika Halmashauri zenyewe husika kwa sababu ni maeneo ambayo wako nayo na wanayatambua katika maeneo yao. Kwa hiyo, haya hayasubiri ule upimaji wa Kitaifa ambao unaendelea kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni Halmashauri zenyewe ziweze kulinda maeneo yake na kama hiyo haitoshi, tumekwishaanza zoezi kwa Dar es Salaam ambapo Wenyeviti wa maeneo husika wamepewa ramani za maeneo yao kuweza kutambua maeneo yapi ya wazi, yapi ya umma na yapi ambayo yanatakiwa kuangaliwa ili yasiweze kuvamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwakumbushie tu kupitia katika swali la Mheshimiwa Mwassa, halmashauri zote zihakikishe kazi ya upimaji maeneo yanayomilikiwa na Taasisi mbalimbali ifanyike ili kuepusha migogoro ambayo inaendelea kutokea siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ameongelea suala la fidia, nadhani tulishalijibu katika hotuba wakati tunazungumzia na bado nitaendelea kulijibu tu. Ni kwamba, Mfuko wa Fidia umewekwa pale ili kuweza kukaa tayari katika kupitia yale masuala ambayo yatakuwa yana migogoro ambayo haijatatuliwa katika ukamilifu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata h ivyo, Wizara kazi yake siyo kulipa fidia katika maeneo ambayo yanatwaliwa na Wawekezaji au na watu binafsi katika maeneo hayo. Ni jukumu lao kuona kwamba analipa fidia, Wizara imetoa maelekezo, haitaweza kupitisha uthamini wowote utakaoletwa, yale majedwali yatakayoletwa, kabla ya kujiridhisha kwamba kuna pesa ambayo imeshatengwa na ndiyo maana Mfuko huu utakuwa na bodi yake ambayo itafanya kazi zake katika kuhakikisha pia wanajiridhisha na kile ambacho Wizara imeelekeza kabla ya fidia kulipwa au kabla ya watu kuondolewa katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishawaelekeza kama Wizara, hakuna mtu kuondolewa katika eneo lake kabla hajalipwa fidia. Kwa hiyo, hilo ni lazima lizingatiwe kwa wale wanaokuwa na mawazo ya kutwaa ardhi za watu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved