Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Margaret Simwanza Sitta
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 1
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Maswali yangu ni kwamba;
a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini katika kata ambazo hazina mawasiliano ya uhakika ili changamoto ziondolewe nao wapate mawasiliano kama wenzao?
b) Je, ni lini Serikali itaachana na teknolojia ya 2G ili nao waende kisasa 4G na 5G?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote nchini yanapata huduma ya mawasiliano. Kwa upande wa kata ambazo, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inatafuta fedha na fedha zikipatikana tutaenda kufanya tathmini ili kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kipengele cha pili, kuhusu suala la kuondokana na huduma ya 2G; tunapokuwa na 3G ndani yake 2G imo. Tunapokuwa na 4G ndani yake 2G imo, tunapokuwa na 5G kwa sababu ile ni specific kwa ajili ya voice na hizi zingine ni kwa ajili ya data. Hizi zote zitakuwa zinaenda sambamba na kuhakikisha pamoja na kwamba kuna advancement ya teknolojia lakini hatuwezi kuachana na huduma ya sauti.
Mheshimiwa Spika, huduma ya sauti itaendelea kuwepo hivyo, hatutaweza kuachana kwa sasa kwa sababu ulimwenguni kote huduma ya 2G inaendelea kutumika na sisi kama nchi tutaendelea kuhakikisha kwamba kuna wananchi ambao watakuwa wanaendelea kutumia huduma hiyo basi tutahakikisha kwamba miundombinu ya huduma hiyo itaendelea kuwepo. Ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Mbunge, nadhani alitaka kujua hiyo huduma ambayo inatolewa sasa, ukiacha hiyo ya voice kama ulivyosema ya 2G, hizo nyingine zitawafikia lini hao wananchi? Ndilo lililokuwa swali la Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, Serikali kuanzia mwaka 2021 tulitoa maelekezo, miundombinu yetu yote ya minara ya mawasiliano inayojengwa, lazima iwe na huduma ya 2G na 3G. Hakuna mnara kuanzia mwaka 2021 ambao umejengwa ukiwa na huduma ya 2G pekeyake.
Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika jimbo lake la Urambo ambalo hata mimi nimepata kutembelea katika kata zake 12, katika kila mnara unaojengwa sasa hivi Urambo una huduma ya kutoa internet. Nakushukuru sana.
Name
Aleksia Asia Kamguna
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 2
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Halmashauri ya Mlimba, Kata ya Uchinjile hakuna kabisa mawasiliano ya simu. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika kata hiyo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimeshafika Mlimba na katika kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ni kwamba tayari imeingizwa katika miradi 758. Zaidi ya hapo, Jimbo la Mlimba tumewapelekea minara saba ambapo tunaamini kwamba itakapojengwa basi utatuzi wa changamoto za mawasiliano utakuwa umefikia ukomo. Ahsante sana.
Name
Esther Lukago Midimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 3
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itafikisha Mkongo wa Taifa Mkoa wa Simiyu?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ni Mkoa wa Simiyu pekee ambao haukuwa umeunganishwa na Mkongo wa Taifa lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha zimeshapatikana na tayari Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa kutoka Shinyanga kupita Bariadi kuelekea Bunda umeshaanza.
Name
Vita Rashid Kawawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Namtumbo
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 4
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kupeleka mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Mgema, Mtelamwai, Mtonya na Masuguru, Wilayani Namtumbo? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba kumekuwa na changamoto ya namna gani Serikali inaenda kutekeleza Mradi wa Tanzania kidigitali hasa katika Miradi ya Minara 758 ambayo imesainiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, tayari utekelezaji umeshaanza lakini ni kwamba kinachofanyika sasa hivi ni upatikanaji wa maeneo yale ambayo yanaenda kujengwa minara na baadaye vibali vipatikane kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, utekelezaji huo unafanyika. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na nimtoe wasiwasi kabisa. Pindi miradi hiyo itakapoanza kujengwa kwa haraka na itakamilika kwa wakati bila kuwa na shida yoyote. Tumewapatia miezi 18 kuhakikisha kwamba wanakamilisha miradi yote, ahsante sana.
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 5
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Serikali ilishatupa taarifa Wabunge juu ya uwepo wa minara hiyo 758; je, ni lini sasa Wabunge tutapata taarifa rasmi na kuzirudisha kwa wananchi kwamba kazi hiyo inaanza? (Makofi)
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tumeingia mikataba na mikataba ya utekelezaji wa miradi hii ni kuanzia miezi tisa mpaka miezi 20. Kwa sababu muda wa mkataba ndio ambao Serikali tunaosimamia, tunahakikisha kwamba ndani ya muda wa makubaliano watoa huduma wote, kulingana na idadi ya minara ambayo waliipata, miradi hiyo iwe imekamilika ndani ya muda wa mkataba, ahsante sana.
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 6
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kule Sikonge tunayo minara kama mitano hivi ambayo ina nguvu ndogo sana yaani coverage yake ni eneo dogo sana. Je, ni lini Serikali itaelekeza haya makampuni waboreshe coverage ya minara yao hasa kwenye Kijiji cha Ibumba?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakunda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kuna timu ambayo iliundwa na Mheshimiwa Waziri na inazunguka kufanya tathmini ili kujiridhisha na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kuna minara ambayo ilijengwa miaka ya nyuma ambapo mahitaji yake ilikuwa watu labda 2,000 au 3,000. Sasa unakuta kwamba katika eneo fulani kuna ongezeko la wakazi 5,000 mpaka 6,000 kiasi kwamba inazidiwa. Kuna miradi mingine ambayo changamoto yake ni masafa, lakini kuna miradi mingine changamoto yake ni teknolojia iliyotumika. Kwa hiyo timu hii inapopita na kujiridhisha chanzo cha tatizo ni nini, ili Serikali ikachukue hatua stahiki kulingana na tatizo la eneo husika. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Kakunda eneo lake tayari alishanijulisha na tayari tumeshaliweka katika utekelezaji wa utafiti huo. Watakaporudi wataalam wetu tutajua kwamba tunaenda kuchukua hatua gani ili tutatue tatizo kulingana na hali halisi iliyopo katika eneo husika, nakushukuru sana.
Name
Shabani Hamisi Taletale
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini Mashariki
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 7
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali italeta mawasiliano katika Kata ya Gwata, Tununguo na Tomondo?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Gwata ipo katika utekelezaji na tusubiri Mheshimiwa Mbunge mradi huu ambapo ukiwa unaendelea kutekelezwa ndani ya kipindi cha mkataba, tunaamini Kata ya Gwata itakuwa imefikishiwa huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
Name
Ally Anyigulile Jumbe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 8
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itaiondoa Wilaya ya Kyela kwenye adha ya mawasiliano yake kuingiliwa na Mtandao wa Malawi?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mbunge wa Kyela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunafahamu kwamba mawasiliano ni uchumi, mawasiliano ni usalama na mawasiliano ni huduma ya msingi ya kila Mtanzania. Sasa wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha tunaona ni busara kuwaacha kwanza wananchi wetu waishi katika mazingira ambayo wanaweza kuwasiliana. Pindi fedha zitakapopatikana, ndipo sasa tutakapoenda kuweka miundombinu yetu na kuhakikisha kwamba sasa mitandao ya nchi jirani tunaiondoa ili waweze kutumia mitandao ya nchi yetu, ili waweze kuchangia uchumi ndani ya Taifa letu na vilevile wawe na usalama ambao unajitosheleza katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali ina mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba tunakuja na mradi maalum wa borders and special zone kuhakikisha kwamba changamoto hii inaisha ili Watanzania wawe na amani ndani ya nchi yao.
Name
Boniphace Nyangindu Butondo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kishapu
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 9
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika mikataba iliyosainiwa ya wakandarasi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya minara, nina minara tisa katika Wilaya ya Kishapu, lakini hadi sasa minara hiyo haijaanza kufanyiwa kazi; je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi hii?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Butondo Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, kwanza Mheshimiwa Butondo alikuwa na tatizo kubwa sana, akaleta na Serikali ikaipokea maombi yake na tukampelekea minara tisa9 kama ambavyo ametaja. Sasa kusaini mkataba ni jambo la kwanza. Jambo la pili, watoa huduma wanaenda ndani ya Jimbo la Mheshimiwa Butondo ili kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga hiyo minara. Wakishapata eneo wanakuja kutafuta vibali kwa mfano kibali cha mazingira (environmental impact assessment permit), kibali cha anga (aviation permit) vilevile wanatafuta kibali cha kutoka halmashauri kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo mlolongo wa vibali hivi, kila sehemu ukikuta kwamba wanatoa kwa uharaka basi mkandarasi ataweza kuanza ujenzi kwa haraka, lakini kukiwa na delay katika baadhi ya maeneo, ndipo inatokea kwamba tunasaini mkataba lakini miezi mitano unakuta kwamba mradi haujaanza.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeshaliona hilo, tunawaomba wote ambao wanahusika katika mnyororo mzima wa utoaji wa vibali, watoe kwa wakati ili kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati kwa sababu Watanzania wanahitaji huduma ya mawasiliano ili washiriki katika uchumi wa kidigitali. Ahsante sana.
Name
Yahya Ally Mhata
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Primary Question
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu katika maeneo ambayo orodha yake iliwasilishwa Wizarani – Urambo?
Supplementary Question 10
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kwenye Wilaya yangu ya Nanyumbu tulipatiwa minara tisa, lakini kuna kata ambayo ina changamoto kubwa haipo ndani ya minara hiyo tisa.
Je, Serikali haioni haja kuleta mnara mmoja kwenye Kata ya Likokona ambayo kuna changamoto ya mawasiliano?
Name
Kundo Andrea Mathew
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu kabisa kwamba, Kata ya Likokona ina changamoto hiyo, mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tulishafika katika maeneo hayo, lakini Serikali ilipokea kata hiyo na katika miradi inayotarajiwa kuja katika ile minara 600, kata hiyo tumeiingiza. Kwa hiyo tumwombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuiombea Serikali iweze kuendelea kupata fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya mawasiliano nchini, ahsante sana.