Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kunti Yusuph Majala
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa stendi ya Wilaya ya Chemba?
Supplementary Question 1
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Suala la andiko tayari Wilaya ya Chemba mwaka 2020/2021 tulishaandika hilo andiko na likaenda TAMISEMI na TAMISEMI wakatushauri tuanze kwa mapato yetu ya ndani. Mpaka sasa tumeshatumia zaidi ya milioni 36 kwa ajili ya ulipaji wa fidia pamoja na kufanya usafi katika eneo hilo. Sasa tunataka kujua, je, ni lini Serikali inakwenda kutekeleza maagizo yake kwenye suala zima la ujenzi wa stendi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, stendi hii pia mwaka 2020 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli alipopita Wilaya ya Chemba wananchi wa Wilaya ya Chemba walimwomba ujenzi wa stendi hii na akaahidi itajengwa haraka iwezekanavyo. Sasa na Mheshimiwa Waziri umesema hapa kwamba mko kwenye mchakato wa kukamilisha ahadi zote za viongozi. Je, ni lini Serikali inakwenda kutekeleza ahadi hii ya Hayati John Pombe Magufuli ili tuweze kumuenzi wananchi wa Wilaya ya Chemba? Ahsante.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, hili la kwanza la andiko. Mpaka sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI haijapokea andiko lolote kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba juu ya ujenzi wa stendi hii, si kusema kwamba Serikali haijapokea, andiko hili huenda liliandikwa likapelekwa moja kwa moja Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafuatilia juu ya andiko hili la Chemba na nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuona andiko hili limefikia wapi na kama kuna marekebisho yoyote, basi yaweze kufanyika na kurejeshwa tena kufanyiwa tathmini ili fedha iweze kutafutwa kadri ya upatikanaji wake kwenda kujenga stendi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la ahadi ya Mheshimiwa Rais, nirejee tena kusema ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha inatekeleza ahadi zote za Viongozi wetu Wakuu wa Nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kadri ya upatikanaji wa fedha na tutaangalia ili tuone tunatenga fedha kwenye mwaka upi wa fedha kadri bajeti itakavyoruhusu.
Name
Jonas William Mbunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Mjini
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa stendi ya Wilaya ya Chemba?
Supplementary Question 2
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango wa kujenga miradi ya kimkakati katika halmashauri mbalimbali, Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni moja ya halmashauri ambayo inatakiwa ipate miradi hiyo ya kimkakati, nataka nijue kupitia mradi wa TACTIC ni lini serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga mradi huo?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya kimkakati upatikanaji wake unaendana sambamba na tutakavyopokea maandiko kutoka kwa wataalam wetu kwenye halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Mbinga na Mradi wa TACTIC alioutaja upo unaratibiwa na Taasisi ya TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona kama TACTIC phase one mradi wa mkakati wote upo katika halmashauri ile, kama haupo tuone ni phase two, kama haupo tuone kama ni phase three, lakini nitumie jukwaa hili la Bunge lako Tukufu kusema tu kwamba kuwaasa wataalam wetu Maafisa Mipango na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa wabunifu wanapofanya maandiko haya ya miradi ya kimkakati. Lengo la Serikali kutoa miradi hii ya kimkakati ni ili halmashauri ziweze kupata uwezo wa kimapato, wasibuni tu mradi ili mradi halmashauri fulani imefanya na wao wakataka, waangalie jiografia yao, eneo lao, ni mambo gani ambayo wakiyafanya basi miradi hii itawaingizia kipato.
Name
Condester Michael Sichalwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Primary Question
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa stendi ya Wilaya ya Chemba?
Supplementary Question 3
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Momba ni miongoni mwa halmashauri 56 ambazo zimewekwa kwenye kundi ambalo tutapangiwa hela za maendeleo asilimia 20. Je ni upi mkakati wa TAMISEMI kutujengea stendi kwenye Kata ya Kamsamba ukanda wa chini, Kata ya Ikana ukanda wa juu kwa sababu sehemu zote hizi zinaunganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Rukwa na kuna uhitaji kubwa sana wa stendi ili zitumike kaka chanzo cha mapato kwenye halmashauri.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Sichalwe amekuwa akilifuatilia sana hili na amekuja mara kadhaa Ofisi ya rais TAMISEMI kulifuatilia hili jambo na tutaendelea kutenga fedha kadri ya upatikanaji wake ili tuweze kuwajengea wananchi wa Momba stendi hizi na kuiwezesha Halmashauri ya Momba kuwa na uwezo wa kupata fedha ya mapato kutokana na miradi hii.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved