Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dennis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: - Je, ajali ngapi za barabarani zimetokea kati ya Mikumi na Ruaha Mbuyuni kwa Mwaka 2010 hadi 2022?
Supplementary Question 1
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Juzi kulikuwa na ajali ambayo imepoteza maisha ya watu watano na majeruhi hali zao ni mbaya; jana kulikuwa na ajali ambayo imejeruhi majeruhi wanane ambao hali zao ni mbaya; na hizi namba ambazo tunapewa na Serikali 128 ni namba za ajali ambazo ni kubwa mno, zina madhara makubwa:-
Mheshimiwa Spika, Swali langu kwa Serikali:-
(a) Serikali haioni wakati umefika sasa kwa sababu ajali hizi zina athari kubwa na pana kwa jamii yote, kutangaza eneo hili kama ni janga?
(b) Serikali haioni wakati umefika sasa Wizara ya mambo ya ndani kukaa pamoja na TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Mtakatifu Kizito kama maeneo ya kimkakati ya uokozi wa majeruhi ambao unatokana na ajali hizi, badala ya kukichukulia kama wanavyokichukulia sasa hivi?
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli ajali hutokea na kadiri alivyosema, katika kipindi cha miaka hii 12 zimetokea ajali 128. Kwa takwimu zetu, ajali hizi zimekuwa zikishuka kadiri Serikali inavyoimarisha usimamizi wa sheria. Kwa mfano, mwaka 2010 tulikuwa na ajali 16 na majeruhi wakawa saba, vifo vinane; 2011 tulikuwa na ajali 14, vifo vitano na majeruhi 10, lakini kadiri miaka ilivyoongezeka ajali hizo zilipungua. Kwa mfano, mwaka 2021 ajali tano, vifo vitatu na majeruhi watatu; na mwaka 2022 ni ajali tano, vifo vitatu na majeruhi wawili.
Mheshimiwa Spika, kiukweli hata kama atakufa mtu mmoja, kwetu tusingependa kumpoteza kwa jambo ambalo lingeweza kuzuilika. Kwa hiyo, pamoja na dhamira yake kwamba litangazwe janga, sijaona kama kiwango hiki kinatufikisha mahali pa kutangaza kama hili ni janga.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutaendelea kuimarisha doria kama inavyofanyika kwa wenzetu wa Iringa, Askari hufuatilia magari haya, na kwa kweli kule ajali zimepungua sana. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu, tumwelekeze RPC Morogoro aanzishe utaratibu kama uliofanywa na mwenzie wa Iringa kuona kwamba magari yanafuatiliwa kwenye maeneo ambayo ni prone, yenye mwelekeo mkubwa wa ajali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kukaa pamoja kwa Wizara husika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kupitia ushirikiano wetu kwenye vikao vyetu vya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, wadau wote aliowataja ni Wajumbe ili kuona namna ya kuimarisha huduma za uokozi katika Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Kizito iliyopo pale Mikumi. Nashukuru sana.
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: - Je, ajali ngapi za barabarani zimetokea kati ya Mikumi na Ruaha Mbuyuni kwa Mwaka 2010 hadi 2022?
Supplementary Question 2
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika harakati za kuimarisha doria, Kituo cha Polisi cha Ruaha Mbuyuni hakina gari: Je, Serikali ina mpango gani wa kukipatia kituo hicho gari ili kuimarisha doria katika eneo hilo lililotajwa ili kupunguza ajali pia? (Makofi)
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli siyo vituo vyote vya Polisi vina magari. Tulichokifanya ni kuimarisha uwezo wa Makamanda wa Mikoa na wasaidizi wao kuwa na magari, lakini awamu inayofuata ni kuimarisha ngazi za Wilaya. Mheshimiwa Nyamoga Wilaya yako itapata gari kama haikuwa na gari la uhakika na tutakapoimarisha kwenye ngazi ya Wilaya tutaenda kwenye vituo vikubwa kama vya Ruaha Mbuyuni ili tuviimarishe. Kwa hatua za dharura tunaweza tukawapatia pikipiki za kuweza kuwawezesha wao kufanya ufatiliaji, nashukuru sana.
Name
Boniphace Mwita Getere
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Primary Question
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: - Je, ajali ngapi za barabarani zimetokea kati ya Mikumi na Ruaha Mbuyuni kwa Mwaka 2010 hadi 2022?
Supplementary Question 3
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Bunge lako lilitunga sheria ya kutoza faini ya boda boda shilingi 10,000 kwa kosa ambalo mwendesha boda boda amefanya. Siku hizi kumetokea matatizo, boda boda sasa hawatozwi faini ya shilingi 10,000, badala yake wanapelekwa Mahakamani kutozwa faini ya shilingi 30,000. Nini tamko la Serikali kuhusu jambo hili?
Name
Sagini Jumanne Abdallah
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli hii faini anayoisema ya Shilingi 10,000/= ni ya papo kwa hapo, lakini wakati mwingine Polisi wanatathmini ukaidi na uzoefu wa hawa vijana kufanya makosa makubwa ya barabarani na hivyo huwapeleka Mahakamani ili Mahakama ambacho ndiyo chombo cha mwisho katika utoaji wa haki watoe hukumu kulingana na uzito au uzembe unaosababisha ajali.
Mheshimiwa Spika, kama amepelekwa Mahakamani na Mahakama imeamua vile, nadhani Mheshimiwa Mbunge tukubaliane. La muhimu ni kuwahimiza vijana wetu waepuke kufanya makosa wanayoweza kuyaepuka ambayo mengi yanasababisha ulemavu na vifo miongoni mwao, nashukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved