Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Vincent Paul Mbogo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kusini
Primary Question
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga barabara ya Ninde, Masokolo hadi Lupata katika Kata ya Kuzumbi?
Supplementary Question 1
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Vijiji vya Lusembwa, Ng’undwe, Mlambo, Minza na Ifinga vinashindwa kupata huduma ya maji, miradi ya maji, mawasiliano pamoja na minara ya simu.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara katika hivi vijiji ambavyo viko Kata ya Wampembe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kata ya Wampembe na Kata ya Kala kuna vilima ambavyo ni korofi, vinasababisha magari ya abiria kutopita; je, ni lini Serikali itajenga kwa zege katika vilima hivi? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo, la kwanza, hii barabara ya Ng’undwe – Mlambo – Lusembwa – Mvinza na Ifinga vilivyokuwepo kwenye Kata hii ya Wampembe, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, barabara hizi zilikuwa bado hazijafunguliwa na kuingizwa kwenye mtandao wa TARURA. Hivyo basi, muda siyo mrefu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nkasi atapita kufanya tathmini ya barabara hizi na kuona ni kiasi gani kinatakiwa kutengwa ili barabara hizi ziweze kuchongwa na greda, na kadiri miaka inavyoenda na fedha kuruhusu basi nazo ziweze kuanza kuwekewa changarawe ili wananchi waweze kupita wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu barabara inayounganisha Kala na Wampembe, kwamba ina vilima vingi, nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Meneja wa TARURA Nkasi, kuweza kufika katika barabara hii ya Kala na Wampembe na kuanza tathmini, na kuona ni kiasi gani kinahitajika kwa ajili ya kuweka zege katika vilima hivi ili barabara hizi ziweze kuwa zinapitika wakati wote wa mvua na hata kipindi ambacho hakuna mvua.
Name
Simon Songe Lusengekile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Primary Question
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga barabara ya Ninde, Masokolo hadi Lupata katika Kata ya Kuzumbi?
Supplementary Question 2
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Barabara ya kutoka pale Nyasho kupitia Mwanangi – Badugu kwenda Busami imekuwa ikiharibika mara kwa mara na ni ya muhimu sana katika uchumi wa Jimbo la Busega: Je, lini Serikali iko tayari kujenga barabara hii kwa kiwango cha changarawe? (Makofi)
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Songe la barabara zake kule Jimboni Busega, wote ni mashahidi kwamba TARURA sasa imeongezewa fedha mara tatu na Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, na bajeti ile imebaki pale pale katika kiwango cha juu cha zaidi ya Shilingi bilioni 776 ambayo Bunge hili lilipitisha. Hivyo basi, niwatoe hofu Wabunge wengi kwamba sasa tunakwenda kufungua barabara nyingi zaidi za mijini na vijijini na vile vile kukarabati barabara nyingi zaidi zikiwemo za kule kwa Mheshimiwa Songe Wilayani Busega.
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Primary Question
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga barabara ya Ninde, Masokolo hadi Lupata katika Kata ya Kuzumbi?
Supplementary Question 3
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara ya kutoka Liweta mpaka Mpopoma ni barabara ambayo ni muhimu sana kiasi kwamba inatenga hicho kijiji kuwa katika mawasiliano na Wilaya ya Nyasa ambayo ndiyo wilaya yake.
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kipekee kuisaidia barabara hii ambayo pia ina milima kama ilivyo barabara ya Wampembe?
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya la barabara hii ambayo inapita Liweta – Mpopoma kule Wilayani Nyasa, nayo vilevile nichukue nafasi hii kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Nyasa kwenda kwenye barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Engineer Manyanya na kuifanyia tathmini na kuona ni kiasi gani kitahitajika kwa ajili ya kuweza kujenga ili tuweze kutengea fedha katika miaka ya fedha ambayo inafuata.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved