Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kupitia Bajeti ya Serikali Kuu?

Supplementary Question 1

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa posho ya Waheshimiwa Madiwani inayotumika hivi sasa ni shilingi 350,000 imekaa takribani miaka kumi sasa.

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza posho ya waheshimiwa Maadiwani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa halmashauri nyingi nchini zinapata mapato madogo, ikiwemo halmashauri ya Mbulu, na kushindwa kulipa posho ya wenyeviti wa vijiji na mitaa;

Je, Serikali haioni kuwa ndio wakati muafaka wa kutazama jambo hili ili kila halmashauri nchini zitekeleze takwa hili la kikanuni kwa mujibu wa huduma wanazotoa?

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issaay, kwanza kuhusu hili la posho kuwa zimekuwa ni za muda mrefu. Mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Serikali kuu ilichukua jukumu la kulipa posho hizi Madiwani moja kwa moja kutoka hazina, hivyo, kuwapunguzia mzigo mamlaka hizi za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupunguza hilo, na kwa sababu ni jambo la kisheria na Mheshimiwa Issaay ni Mheshimiwa Diwani kwenye halmashauri yake ilitakiwa wakae ili zile fedha am,bazo wanafanya saving baada ya Serikali Kuu kuchukua la kulipa posho za Madiwani waone ni namna gani wanatenga kwa ajili ya wenyeviti wao wa vijiji na wenyeviti wao wa mitaa n.k.

Mheshimiwa Spika, pia, fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa kutoka Serikali kuu. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi kwenye miundombinu, afya na elimu. Hivyo, halmashauri nyingi zimepunguziwa ule mzigo mkubwa. Ni wajibu wao kutenga na kuhakikisha wanalipa kama inavyosema Sheria ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nikimalizia kujibu swali lake la kwanza la nyongeza, mwaka huu wa fedha tunaokwenda kuuanza wa 2023/2024 Serikali Kuu vile vile, imewapunguzia mzigo halmashauri zote nchini kwa kuanza kulipa zile stahiki za wakuu wa idara, na zitaanza kulipwa moja kwa moja na Serikali kuu. Hivyo, kuwaacha halmasahuri kuwa na uwezo wa mapato zaidi na kuweza kutenga fedha za kulipa wenyeviti hawa na madiwani vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, linalohusu mapato kuwa madogo. Halmashauri huanzishwa kwa mujibu wa sheria; na moja ya kigezo kikubwa cha uanzishwaji wa halmashauri au mamlaka za Serikali za mitaa ni uwezo wake wa kukusanya mapato. Vile vile, huwa wanaainisha vyanzo zaidi ya 30. Na kwa mujibu wa Sheria ile Na. 287 ya Mamlaka za Wilaya, 288 Mamlaka za Miji inaelezea wazi. Vile vile, Sheria ile ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Kifungu cha (6) (7) (8) na (9) inaelezea wazi namna ambavyo wanatakiwa kubanana kuweka mapato yao sawa.

Mheshimiwa Spika, ukisema kila kitu kichukulliwe na Serikali Kuu ina maana dhana nzima ya D by D inakuwa imeondoka.