Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Miraji Jumanne Mtaturu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga majosho katika Kata za Kolo, Kingale na Bolisa?
Supplementary Question 1
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kondoa, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu majosho haya yanalenga katika kuboresha afya za mifugo ambayo mwisho wa siku tunapata kitoweo kizuri. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba ujenzi huo unasimamiwa vizuri na majosho yale yakamilike kwa muda uliopangwa?
Swali la pili, kwenye Jimbo la Singida Mashariki katika Kata ya Siuyu tulikuwa na josho ambalo sasa hivi limeingiliwa na eneo la Kanisa la RC pale Siuyu na tuliomba lihamishwe liende eneo lingine kwa sababu linakosa sifa ya kutumika pale. Tumeshatenga eneo katika Kijiji cha Siuyu na tuliomba muda mrefu zaidi ya miaka mitatu sasa. Ni lini Serikali itajenga josho kwa ajili ya kutoa huduma ya mifugo katika Kata ya Siuyu. Ahsante sana. (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba amepongeza hii jitihada ambayo tumeifanya lakini vilevile ametaka kuona kwamba kunakuwa na usimamizi mzuri na kuhakikisha haya majosho yanakamilika ili kuimarisha afya ya mifugo. Kwa hiyo, nimuondoe hofu kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Ulega pamoja na mimi Msaidizi wake tunaahidi kabisa kwamba haya yote yaliyopangwa katika mwaka wa fedha unaokuja na yale ambayo hayajakamilika tutahakikisha katika mwaka wa fedha unaokuja yanakamilika kwa wakati kwa sababu hili ndiyo lengo letu na ndiyo lengo la Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa josho katika Kijiji cha Siuyu ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja hapa basi naomba jambo hilo nilipokee kwa sababu nitaangalia katika orodha ambayo tunayo hapa kama tumelitenga katika mwaka huu fedha na kama halipo tuone namna gani tunatafuta fedha ili kuliweka katika moja ya vipaumbele vyetu. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Zuberi Mohamedi Kuchauka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Liwale
Primary Question
MHE. MIRAJI J. MTATURU K.n.y. MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga majosho katika Kata za Kolo, Kingale na Bolisa?
Supplementary Question 2
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Wilaya ya Liwale ndiyo Wilaya katika Mkoa wa Lindi imepokea wafugaji wengi sana lakini hakuna miundombinu ya majosho wala malambo. Je Serikali iko tayari kutujengea majosho na malambo kwenye Kata ya Lilombe na Kata ya Ndapata, Kata ambazo ndizo zimetengwa kwa ajili ya kupokea wafugaji? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Liwale ni miongoni mwa Wilaya ambazo zipo katika mpango wetu katika huu mwaka. Kikubwa tutaangalia katika orodha ili tuone maeneo gani ambayo tutayapa kipaumbele. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved