Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua viongozi wa Vyama vya Msingi waliodhulumu fedha za wakulima wa kahawa Mbozi?

Supplementary Question 1

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kidogo yanatia moyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza wezi wa kuku, wezi wa ng’ombe na mbuzi wakikamatwa wanafikishwa mahakamani, na kufungwa jela, lakini hawa wa Vyama vya Ushirika wanaambiwa tu warudishe fedha na ndio sababu hili tatizo limeota usugu sana Wilayani Mbozi. (Makofi)

Sasa ni lini hawa viongozi watafikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Afisa Ushirika ambaye ametajwa kwenye hii tuhuma kwamba alishirikiana na hawa viongozi wa Vyama vya Ushirika nashangaa mpaka sasa hivi bado yuko kazini, sasa ni lini na yeye hatua hii itamchukulia? Ahsante.

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya uchunguzi taarifa hii imekabidhiwa kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na vyombo vingine vya kisheria kwa ajili ya kuweza kuchukua hatua na ninavyozungumza hivi sasa tayari zaidi ya shilingi milioni 77.6 zimerejeshwa na baadhi ya viongozi wameondolewa na wengine tumewakabidhi TAKUKURU kwa ajili ya hatua za kijinai.

Mheshimiwa Spika, hivyo kazi yetu ilikuwa uchunguzi tumekamilisha, tunasubiri vyombo vingine vya Serikali na vyenyewe vifanye kazi, lakini tu niseme katika hili tumekuwa tukitoa maelekezo mbalimbali, hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atafanya ubadhirifu katika Vyama vya Ushirika na kuwakosesha wakulima mapato yao, Serikali ipo macho tutachukua hatua na hakuna ambaye atapona. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge taarifa iko pale, vyombo vitafanya kazi yake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Afisa Ushirika ambaye yuko chini yetu kwa sababu hii taarifa imeshawasilishwa ili kuendana na uwezo wetu tutachukua hatua stahiki pale ambapo itabainika kupitia taarifa ambayo imewasilishwa kwamba ni mhusika moja kwa moja huyu yuko ndani ya uwezo wetu tutachukua hatua stahiki juu yake.

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Primary Question

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua viongozi wa Vyama vya Msingi waliodhulumu fedha za wakulima wa kahawa Mbozi?

Supplementary Question 2

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa katika msimu wa mwaka jana ambao unaishia sasa hivi baadhi ya wakulima wa zao la kahawa wanavidai Vyama vya Ushirika vingi tu ambavyo bado havijawalipa. Lipi tamko la Serikali kuhusiana na madai hayo ya wakulima?

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, biashara ya mazao ni biashara kama biashara nyingine yoyote. Vyama vya Ushirika vyote ambavyo havijafanya malipo kwa wakulima vinapaswa kufanya malipo kwa wakulima kwa wakati ili kumsaidia mkulima huyu aendelee na shughuli zake za kilimo, hivyo natumia jukwaa hili la Bunge lako tukufu kuwataka wale wote ambao hawajafanya malipo kwa wakulima wafanye mara moja ili kuwaruhusu wakulima kuendelea na msimu unaokuja wa kilimo.