Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jonas William Mbunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Primary Question

MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha changarawe barabara ya Mbinga, Kikolo hadi Kihungu ili iweze kupitika wakati wote?

Supplementary Question 1

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, lakini pia niishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya ukarabati wa barabara hiyo mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Naibu Waziri kwamba ni kilometa 14 tu za barabara hizo zimewekwa changarawe na maeneo ya Mbinga ni maeneo ya mteremko na milima, naomba kujua sasa Serikali ina mpango gani wa kuendelea kuweka changarawe katika kilometa zilizobaki pamoja na kuhakikisha kwamba mitaro imetengenezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Barabara ya kutoka Mbinga – Kitanda – Miembeni – Lupilo – Mpepai na Mtua iliharibika sana hasa katika kipindi cha mvua, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inatengenezwa? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, hii barabara ambayo ni Kitanda Road yenye urefu jumla ya kilometa 32. Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza kilometa sita kwa kiwango cha kifusi. Kama nilivyosema awali tayari ilikuwa imeshatengenezwa kilometa 14 na katika mwaka wa fedha unaofuata Serikali itatengeneza kilometa sita na kuweka mifereji katika maeneo ambayo huwa maji yanajaa.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la barabara hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha huu unaoanza 2023/2024, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuweka concrete (zege) katika yale maeneo korofi ya milimani kwa sababu jiografia ya kwa Mheshimiwa Mbunda kule ni ya vilima vingi. Kwa hiyo tutaweka concrete katika maeneo korofi na vilevile nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunda kwamba ana Barabara hii ya Utili – Mahande ambayo ina kilometa 14 inaenda kuwekewa lami kama ambavyo aliomba yeye kwenye Mradi ule wa Agri–connect.