Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 14 Sitting 12 Youth, Disabled, Labor and Employment Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 192 2024-02-14

Name

Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kwenda kuhakiki wastaafu kwenye Wilaya zao kuliko ilivyo sasa kuhakikiwa mikoani?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza ninaanza kwa kumshukuru na kumpongeza aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Ndugu Hosea Kashimba (CPA) ambaye amemaliza muda wake. Pia, tunamkaribisha sana DG mpya Ndugu Abdul-Razaq Badru, ambaye ameteuliwa hivi karibuni. Tutampa ushirikaano kama Ofisi ya Waziri Mkuu na tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa ambao ameendelea kuutoa akiwa katika Bodi ya Mikopo na sasa kuja kuongoza Mfuko huu. CPA Kashimba, tunamwombea Mwenyezi Mungu amjalie katika majukumu mapya atakayopangiwa. Sisi wote tupo kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, tutaendelea kuwajibika na kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa uaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia swali lake, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Mifuko ya Pensheni nchini imejiwekea utaratibu wa kuhakiki wastaafu wake kwenye mikoa, wilaya au mahali popote wanakoishi kwa kutumia Mifumo ya TEHAMA kila baada ya miezi 12. Katika kuongeza ufanisi, mwaka 2022 Mifuko ya Pensheni iliboresha mifumo ya uhakiki wa wastaafu kwa kutumia alama za vidole (Biometric Verification) ambao ndiyo unaotumika kwa kiais kikubwa kupitia programu ya PSSSF Kiganjani na Dirisha Maalum la Wanachama (Member Portal) lililoko katika tovuti ya Mfuko. Kwa utaratibu huu wastaafu wanahakikiwa mahali popote walipo bila kulazimika kwenda katika Mamlaka za Mikoa kama ilivyokuwa hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho hayo, Mfuko wa PSSSF una mpango wa kuweka vifaa vya uhakiki vya kutumia alama za vidole katika Ofisi za Halmashauri ili kurahisisha zaidi zoezi la uhakiki kwa wastaafu ambao hawatakuwa na uwezo wa kutumia njia za kielekroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kusimamia maboresho katika utoaji huduma kwa wastaafu ili kupunguzia changamoto za kusafiri umbali mrefu kufanya uhakiki na kuwapunguzia gharama zisizo za lazima wastaafu husika, ahsante.