Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 15 Sitting 29 Finance Wizara ya Fedha 387 2024-05-20

Name

Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha mfumo mzuri wa kutoa msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaojenga barabara Halmashauri ya Msalala?

Name

Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, msamaha wa kodi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kimkakati ya Serikali unatolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT kama ilivyofanyiwa maboresho na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho ya sheria hiyo yalilenga kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji wa msamaha wa kodi ambapo awali mamlaka ya kutoa msamaha yalikuwa chini ya Waziri wa Fedha. Aidha, kwa marekebisho hayo, mamlaka ya kutoa msamaha yakakasimishwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho ya sheria, Serikali kupitia TRA, ilianzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kushughulikia misamaha ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Kuanzishwa kwa kitengo hicho kumesababisha kuwa na muda mfupi zaidi wa kushughulikia maombi ya msamaha wa kodi hiyo ukilinganisha na wakati wa awali kabla ya maboresho hayo. Vilevile katika jitihada za kuongeza ufanisi na kutoa msamaha wa kodi ndani ya muda mfupi, Serikali ilianzisha mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maombi hayo TRA (Tax Exemption Management System), ahsante. (Makofi)