Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 18 | Sitting 6 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 103 | 2025-02-04 |
Name
Deodatus Philip Mwanyika
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Primary Question
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itachukua hatua za kuhakikisha uvunaji wa rasilimali misitu unazingatia uongezaji thamani?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uvunaji wa rasilimali misitu unazingatia uongezaji wa thamani ya mazao hayo, kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani na soko la nje. Katika kutekeleza mpango huo Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wadau wa mazao ya misitu kuhusu matumizi ya teknolojia ya kisasa katika uongezaji thamani katika mnyororo mzima wa mazao ya misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeanzisha Kituo cha Mafunzo ya Misitu na Viwanda vya Misitu kilichopo Wilayani Mafinga, Mkoani Iringa, ambacho kinatoa mafunzo ya kuongeza thamani mazao ya misitu, hususan Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya vijana 27 wa kozi ndefu na vijana 103 wa kozi fupi wamehitimu, ambao hutumika kutoa mafunzo kwa wakulima wa miti katika mikoa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Mazao ya Mbao yaliyohandisiwa Mwaka 2021 pamoja na Mpango Kazi wake kwa Mwaka (2021–2031). Mpango mkakati huu umesaidia katika kuimarisha uzalishaji na biashara ya mazao ya misitu yaliyohandisiwa, ambapo hadi sasa kuna jumla ya viwanda 48 vinavyozalisha bidhaa ya venia katika Mikoa ya Iringa na Njombe na kati ya viwanda hivyo, viwanda 27 vipo katika Jimbo la Njombe Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara imeandaa kanuni kupitia Tangazo la Serikali Na. 266 la Machi, 2023 linalolenga kusimamia usafirishaji wa bidhaa za mazao ya misitu yanayoingia na yanayoenda nje ya nchi. Aidha, hadi kufikia Desemba, 2024 kiasi cha mita za ujazo 38,056 za bidhaa za misitu zilizongezwa thamani, zenye thamani ya Dola ya Marekani 9,079,813, zilisafirishwa kwenda nje ya nchi.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved