Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, lini Serikali itachukua hatua za kuhakikisha uvunaji wa rasilimali misitu unazingatia uongezaji thamani?

Supplementary Question 1

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali na vile vile tunawashukuru kwa hizo juhudi zote ambazo wanazifanya, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, natambua sasa kwamba, vibali vinaendelea kutolewa kwa wale wazalishaji wa venia katika kipindi hiki ambacho sisi tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba, thamani katika mazao ya misitu inaongezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali. Serikali ipo tayari kutoa masharti kwamba, hata kama hawa wanafanya uvunaji, na nyingi ni kampuni za nje kutoka sehemu za Asia. Je, wanaweza wakawapa masharti kwamba, wavune, lakini wawe na mpango kazi wa kuhakikisha kwamba, wanajenga viwanda vya kuongeza thamani katika mazao haya ya misitu na hasa venia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Hata kwa hicho kidogo ambacho kinachukuliwa kama mazao ya misitu na yanakuwa processed, bei ambayo wakulima wanapewa ni ndogo sana. Tunaiomba Serikali, ni kwa nini isiweke utaratibu wa kutoa angalau bei elekezi ambayo iko fair kwa wakulima wetu wa mazao ya misitu?

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge linakumbuka kwamba, tulikuwa na zuio la kuruhusu usafirishaji wa venia. Serikali ilipata muda wa kuandaa utaratibu mpya ambao sasa unatumika kuwaruhusu wenye viwanda kuweza kuzalisha venia na kusafirisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kupitia utaratibu mpya uliowekwa wote ambao wamepewa leseni za kuzalisha na kusafirisha venia nje ya nchi, wamewekewa utaratibu wa kuhakikisha ndani ya kipindi cha miaka miwili wawe wamejenga uwezo wa kuboresha viwanda vyao ili kuweza kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha hapa ndani ya nchi. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuko vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili. Muda wote tunaongozwa na nguvu ya soko, lakini tumepokea ushauri wake, tunaenda kuufanyia kazi, tutaona jinsi ambavyo tunaweza kuu-accommodate.