Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 18 | Sitting 6 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 104 | 2025-02-04 |
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kuondoa adha ya uvamizi wa tembo katika Kijiji cha Nyabugombe, Kata ya Nyakahura, Biharamulo?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Nyabugombe kilichopo katika Kata ya Nyakahura ni miongoni mwa vijiji 38 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Burigi, Chato. Kwa kipindi cha miezi sita Julai – Desemba, 2024 jumla ya matukio 16 ya tembo yaliripotiwa na kudhibitiwa katika Kijiji cha Nyabugombe kilichopo Kata ya Nyakahura, Wilaya ya Biharamulo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na adha ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo katika maeneo yanayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Burigi, Chato.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kushirikiana na wananchi kudhibiti tembo kwa wakati, ambapo jumla ya Askari sita wa uhifadhi kwa kushirikiana na mgambo sita waliopewa mafunzo kuhusu tabia za wanyamapori wanatumika kufukuza tembo kupitia Kituo cha Nyungwe kilichopo Kijiji cha Nyabugombe, Kata ya Nyakahura.
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari hao wamewezeshwa vitendea kazi mbalimbali, likiwemo gari moja, GPS mbili, tochi muhimu za kufukuzia tembo na mabomu baridi 50. Aidha, wananchi 425 wamepatiwa elimu kuhusu mbinu mbadala za kukabiliana na tembo kupitia mikutano ya hadhara. Vilevile katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi 19,800,000/= kwa ajili ya kuweka uzio wa pilipili katika eneo la Hifadhi ya Burigi, Chato, linalopakana na Kata ya Nyakahura.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved