Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, nini mpango wa Serikali wa kuondoa adha ya uvamizi wa tembo katika Kijiji cha Nyabugombe, Kata ya Nyakahura, Biharamulo?
Supplementary Question 1
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, na ninashukuru kwa ajili ya hao maaskari ambao wameletwa katika eneo la Nyabugombe, especially Kituo kile cha Nyungwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili. Sehemu ya kwanza ni kwamba, pamoja na wale maaskari kuwepo, lakini bado matukio ya tembo kutoka na kupita yamekuwa yanaendelea kiasi kwamba, baadhi ya wananchi wameathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu. Ni lini madai ya wananchi wote wa Nyakahura ambao wameathiriwa na tembo waliotoka ndani ya hifadhi wataweza kulipwa, kwa sababu, ni muda mrefu yapo madai, lakini hayajalipwa na wananchi waliharibiwa mazao ambayo ndiyo chakula wanachokitegemea kwa sababu, hawana shughuli nyingine ya kuwaingizia Uchumi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kipindi kilichopita tukiongea na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitujulisha habari ya kuhamisha tembo zaidi ya 200, kuwatoa kwenye Hifadhi ya Kyerwa na hatimaye wawalete katika eneo letu hili la Burigi. Sasa tunafurahi kwa sababu wanadumisha utalii, lakini wale tembo wanaokuja ni wengi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa twende kwenye swali.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tembo waliopo sasa, bado wamekuwa wanaweza kutoka nje ya hifadhi. Je, mmejiandaaje kukabiliana na ongezeko la tembo zaidi ya 200 wanaohamishwa kutoka Rumanyika kuja Biharamulo kwenye Hifadhi ya Burigi ili iweze kuondoa matatizo ambayo yanawakabili wananchi, hususan uharibifu wa mazao?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, yapo madai ya wananchi ambapo tathmini ya awali iliyofanyika inaonesha kwamba, kiasi cha shilingi 1,675,000/= zinahitajika, kwa ajili ya kuwalipa, lakini vilevile tuko kwenye hatua ya kuhakikisha kwamba, madai haya ndiyo sahihi. Kwa hiyo, tumewasiliana na wenzetu wa halmashauri husika ili kuhakikisha kwamba, taarifa walizotuletea ndiyo halisi na hakuna taarifa nyingine ambazo bado hazijafika. Mara baada ya wao kukamilisha utaratibu huo wananchi hao watalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hili la kukabiliana na tembo ambao tunakusudia kuwahamishia kwenye eneo hili, kama ambavyo tumesema, katika mwaka huu wa fedha tuna mkakati wa kuweka uzio wa pilipili katika eneo linalopakana na hifadhi. Tunataka kutumia mkakati huo kuona jinsi ambavyo unaweza kutumika kufukuza tembo na kama kutahitajika jitihada kubwa zaidi za kuweka uzio wa umeme, basi Serikali haitasita kufanya hivyo.
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA aliuliza: - Je, nini mpango wa Serikali wa kuondoa adha ya uvamizi wa tembo katika Kijiji cha Nyabugombe, Kata ya Nyakahura, Biharamulo?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Mkoa wa Mara wanaoishi kandokando ya Mbuga ya Serengeti wamekuwa wakiathirika na uvamizi huu wa tembo. Sasa, moja ya mkakati wa Serikali, wameainisha pia, ni matumizi ya mabomu baridi ambayo unakuta wamegawiwa baadhi tu ya watu. Serikali haioni kwamba, kuna haja ya kutoa elimu ya matumizi ya haya mabomu baridi ikiwa ni sanjari na ugawaji wa mabomu haya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, twende kwenye swali.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kaya ambazo zinaathirika…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Matiko…
MHE. ESTHER N. MATIKO: …na uvamizi wa tembo hawa, ili waweze kujilinda pale ambapo unakuta wanavamiwa?
Name
Dunstan Luka Kitandula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya mabomu baridi ni moja tu ya njia ambazo tunazitumia katika kukabiliana na madhara ya tembo. Kwenye maeneo ambayo tunaweza kutumia teknolojia ya drone au tunaweza kutumia helikopta, tunatumia njia hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo ambayo tunatumia mabomu, elimu inatolewa kwa wananchi, lakini nguvu kubwa zaidi inaelekezwa kwa wale wanaoyatumia mabomu haya kwa sababu, bila kutoa elimu hiyo tunaweza kupata madhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ambayo wananchi waliamua wenyewe kutumia mabomu bila ya kupata mafunzo, yakaleta madhara. Kwa hiyo, sasa hivi tumezuia kabisa wananchi ambao hawajapewa mafunzo kuweza kutumia mabomu haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa halmashauri zetu ambazo zimekuwa na mpango wa kununua mabomu, kuongeza nguvu kwa yale yanayoletwa na Serikali, wazingatie utaratibu uliowekwa wa kuhakikisha wanaoyatumia wawe ni wale tu ambao wamepatiwa mafunzo.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba kutumia fursa hii kulieleza Bunge letu Tukufu yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la changamoto ya tembo katika baadhi ya maeneo ambayo yanapakana na hifadhi, linapaswa kuwa ni ajenda ya halmashauri husika. Katika vikao vya halmashauri, tuna Kamati ya Madiwani inayoshughulika na masuala ya mazingira. Mfano, baadhi ya maeneo kuna changamoto ya mamba kuumiza wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri husika inapaswa kutenga eneo la kuweka bomba ili wananchi wasichote maji katika eneo ambako kuna mamba. Vilevile, kuna maeneo kuna changamoto ya tembo, halmashauri husika inapaswa kuchukua majukumu yote kulinda wananchi wakishirikiana na sisi Wizara na mashirika yetu ya TAWA na TANAPA. Katika bajeti za halmashauri, asilimia 10 za halmashauri, mapato ya ndani na kuna maeneo tunarudisha fedha za Wildlife Management Area, 25% inarudi katika halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi zinatakiwa zitumike kwa shughuli rafiki, uhifadhi, pamoja na kulinda wananchi wasiumizwe. Hivyo, ajenda ya kulinda wananchi dhidi ya changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja ya wanyama, ni ajenda ya halmashauri husika na full council.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshawasiliana na Mheshimiwa Waziri mwenzangu kwamba, wakati umefika tuelekeze Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wafanye kazi nzuri. Ma-DC na Waheshimiwa Madiwani lazima walijadili hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna halmashauri za kutosha, walijadili, tunalindaje wananchi katika jurisdiction, mamlaka, ya eneo husika? Halmashauri zinaweza kununua drone, halmashauri inaweza kupeleka vijana VGS kusomea namna ya kulinda, tunaita Village Game Scout. Tuna vyuo vyetu vya Likuyu na Sekamaganga, ni lazima tuje na reforms.
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nitoe shukrani sana kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba, sasa tutashirikiana na Kamati za Madiwani kuhakikisha tunalinda wananchi wetu kwa fedha za Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.