Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 19 Sitting 21 Industries and Trade Wizara ya Viwanda na Biashara 271 2025-05-09

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -

Je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka unakamilika?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha mradi huu unakamilika, Serikali inatekeleza mkakati wa utekelezaji wa mradi ambapo iliutangaza mradi huo tarehe 30 Disemba, 2024 na kampuni 28 za ndani na nje ya nchi zilionesha nia ya kuwekeza katika mradi huo. Hadi mwisho wa zabuni tarehe 24 Februari, 2025 ni kampuni ambazo ziliwasilisha zabuni za kushirikiana na Shilika la Taifa la Maendeleo (NDC) kutekeleza mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayoendelea ni kufanya upekuzi (due diligence) ili kujiridhisha kampuni hizo kama zitakidhi vigezo zitapewa tuzo (awards) ya kutekeleza mradi huo kwa kushirikiana na NDC. Mpango huo uliopo baada ya kutoa tuzo na kusaini mikataba, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza ndani ya miezi 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza mradi huo hadi sasa shughuli zifuatazo zimefanyika: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tumeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mradi na faida zake, lakini pili, kufanya utafiti wa awali wa magadi soda na utafiti wa kina wa magadi uliohusisha uchimbaji wa mashimo 16 ya utafiti. Pia kufanya upembuzi yakinifu na kufanya utafiti wa athari za mradi kwa mazingira na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi tulifanya uthamini na kulipia fidia ya zaidi ya shilingi milioni 5.8 ambazo zimelipwa kwa wananchi ili kupisha huo mradi. Pili, tumelipa ada za leseni za mradi huo, zaidi ya shilingi milioni 408 na tumeshautangaza mradi huo kama nilivyosema kwa lengo la kupata wawekezaji. Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kuhakikisha miundombinu ya barabara, maji na umeme inakamilishwa ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.