Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 19 Sitting 13 Defence and National Service Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa 163 2025-04-28

Name

Rose Vicent Busiga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ROSE V. BUSIGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itawalipa mafao yao mashujaa wa Vita vya Kagera na Uganda?

Name

Dr. Stergomena Lawrence Tax

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mashujaa wote waliopigana vita vya Kagera na waliostahili malipo ya viinua Mgongo na Pensheni walikwishalipwa na wengine wanaendelea kulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Pensheni na Viinua Mgongo ya Mwaka 1966; ikiwemo pia malipo ya ulemavu na ustaafu.

Mheshimiwa Spika, kundi ambalo lilishiriki vita na halikuwa limeajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama, baada ya vita lilipewa nafasi ya kujiunga katika vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufuata taratibu. Kwa wale walioamua kutojiunga na wale waliokosa sifa katika kundi hilo walilipwa kifuta jasho, Ahsante Nyerere kiasi cha Shilingi 5,000 ambayo kwa wakati huo ilikuwa pesa ya kutosha na kurejeshwa makwao.

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikikabiliana na changamoto mbalimbali kuhusiana na maveterani wa Vita ya Kagera. Miongoni mwa changamoto hizo ni madai ya mavetenari wote kuingizwa katika daftari la Pensheni licha ya kuwa baadhi yao hawakidhi vigezo kwa mujibu wa Sheria, madai kuwa pensheni ni ndogo na maombi ya kupewa Bima ya Afya.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imeandaa mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Pensheni na Viinua Mgongo ya mwaka 1966 na kuiwasilisha Serikalini, yakijumuisha maveterani waliopigana Vita vya Kagera. Aidha, Wizara imewasilisha Serikalini mapendekezo ya kuona uwezekano wa kuwaingiza maveterani waliopigana Vita vya Kagera kwenye utaratibu wa bima ya afya.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.