Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 7 | Sitting 21 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 182 | 2017-05-10 |
Name
Raisa Abdalla Mussa
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA) aliuliza:-
Kutokana na umuhimu wa misitu hapa nchini na kwa kuzingatia kuwa theluthi moja ya ardhi ya Tanzania ni misitu; na kwa kuwa, Serikali ina Chuo kimoja tu cha Misitu cha Olmotonyi ambacho sasa kinakaribia kufikisha karne moja tangu kianzishwe:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vyuo vingine vitakavyotoa taaluma zaidi ya misitu kwa Watanzania?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raisa Abdallah Mussa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania Bara ina eneo la takribani hekta milioni 48 za misitu sawa na 55% ya eneo lote la nchi kavu lipatalo hekta milioni 88.1. Kwa mujibu wa viwango vinavyoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, inakadiriwa kuwa Afisa Misitu mmoja husimamia wastani wa hekta 5,000 za misitu hivyo, kwa ukubwa wa eneo la misitu katika nchi yetu kiasi cha wataalam wa misitu 9,600 wenye jukumu la kusimamia misitu moja kwa moja ukiondoa watawala na watumishi wa viwandani na kadhalika wanahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina vyuo vitatu vinavyotoa taaluma ya misitu. Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine kilichoko Morogoro ambacho kinatoa Shahada ya Kwanza, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu katika Fani ya Misitu; Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi, ambacho kinatoa Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu na Astashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu na Chuo cha Misitu kilichopo Olmotonyi, ambacho kinazungumziwa na Mheshimiwa Mbunge muuliza swali, nacho kinatoa mafunzo ya Astashahada na Stashahada ya Misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kujali vyuo walivyosoma, taaluma mahsusi ya misitu na ngazi za shahada walizohitimu, katika kipindi cha miaka 10 vyuo nilivyovitaja hapo juu vimeweza kuzalisha jumla ya wataalam 3,500 ambao wameingia kwenye soko la ajira. Kufikia mwaka 2020, Serikali inao mpango wa kuongeza udahili, mara mbili ya viwango vya sasa, katika vyuo vilivyopo kwa kutekeleza, pamoja na mambo mengine, uboreshaji miundombinu ya kufundishia, kuongeza ubora na idadi ya wakufunzi na vifaa vya kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, mipango ya Serikali inaonesha uwezekano mkubwa wa kufikiwa kwa malengo ya kupatikana kwa wataalam wa kutosha kwa idadi na uweledi, kwa sasa Serikali haioni umuhimu wa kuongeza vyuo vingine kwa madhumuni hayo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved