Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Yussuf Salim Hussein
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Chambani
Primary Question
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA) aliuliza:- Kutokana na umuhimu wa misitu hapa nchini na kwa kuzingatia kuwa theluthi moja ya ardhi ya Tanzania ni misitu; na kwa kuwa, Serikali ina Chuo kimoja tu cha Misitu cha Olmotonyi ambacho sasa kinakaribia kufikisha karne moja tangu kianzishwe:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vyuo vingine vitakavyotoa taaluma zaidi ya misitu kwa Watanzania?
Supplementary Question 1
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri, mimi kama mtaalam wa misitu, naomba hili swali lijibiwe tena, halikujibiwa, la kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu haya ambayo wataalam wa Mheshimiwa Waziri wamejaribu kuzunguka, unaposema FITI ni Chuo Cha Misitu, Chuo cha Nyuki kwa nini umekiacha? FITI ni consumers siyo misitu. Tukisema foresters ni yule ambaye unampa mbegu anakupa product ama ya timber ama ya log, huyo ndiyo mwanamisitu, sio unayempa ubao akafanya processing. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, hivi kweli Watanzania tunajiangalia kwamba misitu ina umuhimu kwa maisha yetu na vizazi vyetu na viumbe vingine vilivyomo katika ardhi? Hekta 5,000 kuhudumiwa na mtu mmoja, tuko serious kweli? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, unaposema katika kipindi cha miaka 10…
Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Swali la pili, unaposema una wanataaluma 3,500 katika kipindi cha miaka 10, ni wastani wa 350 kwa mwaka. Hebu tupe mchanganuo kwa sababu katika vyuo vyote darasa halizidi watu 40 na ni madarasa mawili tena ya certificate, wanaochukua degree hawazidi watu 50 kwa siku. Kwa hiyo, mnatoaje watu 350 kwa mwaka? (Makofi)
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, pamoja na maelezo mengi ya utangulizi aliyotoa, nililoweza kulinukuu kama swali mahsusi ni kwamba, inawezekanaje hekta 5,000 zikahudumiwa na mtaalam mmoja wa misitu. Dunia inaendeshwa kwa sayansi na teknolojia, wataalam na miongozo mbalimbali. Mawazo na maoni ya mtu mmoja-mmoja yanaheshimiwa lakini yanatakiwa yakae ndani ya utalaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nasoma jibu langu nimenukuu kwamba takwimu hizi au viwango hivi vimewekwa kimataifa na vimewekwa na Shirika la Chakula Duniani la FAO. Sasa inawezekana Mheshimiwa Mbunge ana maoni mazuri zaidi kuliko yale ya Shirika la Kimataifa la Dunia, basi nafikiri maoni yake hayo afuate channels zinazofaa ili kuweza kwenda kuboresha hali hiyo kwa namna ambavyo ataona inafaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nalo pia ni la takwimu. Anasema inampa mashaka kidogo kuona kama kweli tuna wataalam hao 3,500 kwa kuwa, kwa mujibu wa taarifa alizonazo yeye watalaam wanaozalishwa kwa mwaka kwa vyuo vyote ni 350, sasa ni muda gani utakuwa umepita huo kuweza kupata idadi ya watalaam hawa 3,500. Kwa sababu, hili ni swali linalohusiana na takwimu, swali lake hilo ili niweze kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuweza kumwambia namna gani tumefikia hapo, basi anione kwa wakati muafaka, hata mchana huu nitaweza kumpa mchanganuo mzuri. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved