Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 8 Sitting 1 Natural Resources and Tourism Wizara ya Maliasili na Utalii 11 2017-09-05

Name

Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Primary Question

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Msitu wa Hifadhi ya Taifa Minziro una vivutio vingi vya utalii.
(a) Je, ni watalii wangapi wametembelea msitu huo ndani ya kipindi cha miaka 20 hadi sasa?
(b) Je, wananchi wanaoishi karibu na msitu huo wananufaikaje?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya mwaka 2015, Msitu wa Hifadhi wa Minziro haukuwa miongoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa na kusimamiwa kwa ajili ya shughuli za utalii. Hata hivyo, kwa sasa hifadhi hiyo ipo katika hatua za awali za maandalizi ya mpango endelevu wa kuendesha utalii wa ikolojia katika msitu huo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015 Serikali ilianzisha mradi wa kuboresha uhifadhi wa bionuwai katika hifadhi 12 za misitu ya mazingira asilia zilizopo nchini. Hifadhi hizo zikiwa ni pamoja na Mlima Rungwe kule Mbeya, Udzungwa na Kilombero zinazopakana na Iringa na Morogoro, Uluguru na Mkingu zinazopakana na Morogoro, Amani, Nilo na Magamba zilizopo ndani ya Mkoa wa Tanga, Chome kule Kilimanjaro, Rondo – Lindi na Mlima Hanang Mkoa wa Manyara, chini ya mradi unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Aidha, kutokana na kuwepo kwa mipango ya awali ya kuanzisha utalii wa ikolojia katika hifadhi hiyo, katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015 jumla ya watalii 11 walitembelea hifadhi hiyo ambapo tisa ni raia wa kigeni na wawili ni Watanzania.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi jirani na Msitu wa Minziro kwa kutunza, kuhifadhi na kulinda msitu huu kwa sasa wananufaika kwa kupata vyanzo bora vya maji, hali ya hewa iliyo bora na ardhi yenye rutuba na sifa nyinginezo muhimu kwa kilimo na maisha ya wananchi kwa ujumla. Aidha, katika siku zijazo baada ya kukamilika kwa mpango unaoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu, wananchi hao watanufaika kwa kupata gawio la asilimia 26 ya mapato yatakayotokana na utalii wa ikolojia ambao hufanyika kwa njia shirikishi na wananchi katika kusimamia hifadhi na kuendesha utalii huo.