Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 10 Sitting 9 Justice and Constitutional Affairs Wizara ya Katiba na Sheria 116 2018-02-09

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wanawake wengi bado hawaelewi haki zao hasa kuhusu haki za kumiliki ardhi.
Je, kuna mkakati gani wa Serikali wa kuwawezesha wanawake waweze kujua haki zao za kumiliki ardhi?

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuhusu haki ya wanawake kumiliki ardhi. Elimu hiyo imekuwa ikitolea kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vipindi vya redio na luninga, mikutano ya hadhara, warsha, semina, maonesho mbalimbali kama vile Siku ya Sheria, Wiki ya Utumishi wa Umma, Siku ya Mtoto wa Afrika, Maadhimisho Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, Wiki ya Msadaa wa Kisheria pamoja na maonyesho mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikichapisha machapisho yenye kuelimisha umma kuhusu masuala ya umiliki wa ardhi. Aidha, Tume hiyo imetoa elimu katika Kata 72 katika Wilaya 18 za Tanzania Bara na Shehia nane za Wilaya nne za Tanzania Zanzibar. Wilaya za Tanzania Bara ni Biharamulo, Ngara, Mpanda, Babati, Simanjiro, Mbarali, Mbeya, Mvomero, Ulanga, Ludewa, Makete, Nkasi, Namtumbo, Tunduru, Kahama, Kishapu, Kilindi na Tanga; na Wilaya za Tanzania Zanzibar ni Unguja Kusini, Unguja Kaskazini- A, Mkoani na Michweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuendelea kuelimisha umma katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar hasa kwa wanawake ili wananchi wote waweze kufurahia haki zao za msingi ikiwemo haki ya kumiliki ardhi.