Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:- Wanawake wengi bado hawaelewi haki zao hasa kuhusu haki za kumiliki ardhi. Je, kuna mkakati gani wa Serikali wa kuwawezesha wanawake waweze kujua haki zao za kumiliki ardhi?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, licha ya elimu kutolewa lakini bado kuna matatizo kuhusu haki ya ardhi. Sasa Serikali inaonaje kutoa kipindi maalum, narudia, kipindi maalum kwa muda muafaka kwenye luninga au kwenye redio kusudi elimu hii iwafikie hasa wanawake kwa wakati muafaka na kwa muda muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi inatumiwa sana na wanawake; kama asilimia 70 wanawake wanatumia hii ardhi hasa kwa uzalishaji mali hasa kwa kilimo. Hata hivyo wanawake hawa hawana maamuzi kuhusu ardhi hii. Je, Serikali inatoa kauli gani hasa ya kueneza elimu hii na kutokana na kwamba kwenye makabila mengine bado kuna mfumo dume ambao hauwapi ridhaa wanawake kumiliki ardhi? ahsante.

Name

Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilosa

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Dkt. Christine Gabriel Ishengoma kwa sababu alifanya utafiti mmoja ambao ulikuwa ni utafiti mzuri sana kuhusu mfumo wa kumiliki ardhi kwa watu wanaotoka katika makabila ambayo ni matrilineal au matriarchal. Yaani wale ursine local matriarchal wa makabila ya Pwani kama Wazaramo, Wakwere, Wakutu, Waluguru, Wanguu, Wakaguru lakini pia wale matrilineal ambao ni Wamwera, Wayao, Wamakua, Wamakonde na kuonesha ni jinsi gani katika maeneo hayo mfumo ule ambao sasa sijui ni mfumo jike, lakini umiliki wa ardhi unatoa maeneo ambayo yangesaidia watu wa mfumo dume kujifunza; na labda ndiyo maana katika historia ya Bunge letu wanawake wengi mwanzoni walioshinda Ubunge wa Majimbo walitoka maeneo hayo ya Wamwera, Wayao, Wamakua na Wamakonde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakubaliana naye kwamba kuna umuhimu wa kuwa na kipindi maalum cha mambo ya ardhi katika luninga na redio kwa wakati muafaka ili wanawake wengi wakisikie. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kumuahidi kwamba nitaongea na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kuandaa vipindi hivi kwa wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, niseme tu kwamba tuendelee kuelimishana kuhusu umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi hasa katika maeneo ya mfumo dume. Vilevile pia niwaombe Mahakimu na Majaji wengi waelewe umuhimu na utofauti wa umiliki wa ardhi katika maeneo ya Tanzania ya Pwani na Kusini yenye mfumo jike katika kumiliki ardhi kwa sababu hukumu zao zimekuwa hazielewi kwanini katika maeneo hayo wanawake wana sauti ya maamuzi. Na kwa maana hiyo basi tuendelee kuimarisha jambo hili ili mwisho wa siku jinsia zote mbili ziwe na haki sawa katika umiliki wa ardhi. (Makofi)