Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 30 Energy and Minerals Wizara ya Nishati 260 2018-05-16

Name

Justin Joseph Monko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Primary Question

MHE. JUSTIN J. MONKO aliuliza:-
Mradi wa REA Awamu ya Pili katika Jimbo la Singida Kaskazini ulisimama tangu mwaka 2016 na kukosesha huduma hiyo kwa vijiji vilivyokusudiwa mwaka 2017, utekelezaji wa REA Awamu ya Pili katika vijiji 30 kati ya 64 vilivyokusudiwa umeanza.
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ukamilishaji wa mradi wa REA II?
(b) Je, ni lini mkandarasi wa REA II awamu ya pili atapatikana na kuanza kazi?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Justin Joseph Monko, Mbunge wa Singida Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mradi wa REA Awamu ya Pili katika Mkoa wa Singida ulisimama kutekelezwa mwaka 2016 kutokana na mkandarasi Spencon Ltd. kushindwa kukamilisha kazi zake baada ya kufilisika. Hata hivyo, tayari vifaa vyote vya mradi vilikuwa vimenunuliwa na kuhifadhiwa. Wakala wa Nishati Vijijini wamesaini mkataba mpya na Kampuni ya JV Emec Engineering Ltd. & Dynamic Engineering and System Co. Ltd. wenye thamani ya shilingi milioni 991.6 kwa ajili ya kukamilisha kazi za REA Awamu ya Pili katika Wilaya ya Iramba, Mkalama na Singida Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Wakala wa Nishati Vijijini umesaini mkataba na Kampuni ya JV East African Fossils Co. Ltd & CMG Construction Co. Ltd. wenye thamani ya shilingi 459.23 kwa ajili ya kukamilisha kazi katika Wilaya ya Manyoni. Mikataba yote miwili imesainiwa mwezi Machi, 2018 kwa muda wa miezi sita. Kazi ya kusambaza umeme katika meneo yaliyotajwa zitakamilika mwezi Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza, kazi za mradi zinatekelezwa na Mkandarasi M/S CC- Etern Consortium Ltd. ya China, kazi za Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza katika Mkoa wa Singida zinajumuisha kuvipatia umeme vijiji 150 ambapo Jimbo la Singida Kaskazini litaunganishiwa umeme jumla ya vijiji 30 na kuunganishia wateja wa awali 870. Mradi utakamilika mwezi Juni, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kusambaza umeme katika Mkoa wa Singida kwa miradi ya REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na wa pili zinajumuisha ujenzi wa kilometa 286.1 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, kilometa 568 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transfoma 284 na kuunganishia wateja wa awali 8,659. Kati ya wateja hao, wateja 7,795 wa njia moja na wateja 864 wa njia tatu. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 29.56 na dola za Kimarekani milioni 5.34.