Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 11 | Sitting 48 | Regional Administration and Local Government Authorities | Ofisi ya Rais TAMISEMI. | 407 | 2018-06-11 |
Name
Susan Limbweni Kiwanga
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Mlimba
Primary Question
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba lina vijana wengi wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari na vyuo lakini wanashindwa kujiajiri kwa kukosa elimu ya ufundi kutokana na jimbo kuwa na kituo kimoja cha ufundi stadi kilichopo Shule ya Msingi Mchombe. Hata hivyo, kituo hicho chenye mahitaji ya walimu sita kina walimu wawili pekee na hakina vifaa. Aidha, kituo kilichopo Shule ya Msingi Mpanga hakina walimu wala vifaa:-
(a) Je, ni lini Serikali itaboresha vituo hivyo vya Mchombe na Mpanga kwa kuwapelekea walimu na vifaa?
(b) Vijana wachache wanaomaliza Kituo cha Mchombe na kufanya mitihani ya NECTA hawapewi vyeti. Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu mzuri katika vituo hivyo ili wawe wanapewa vyeti ili waweze kujiendeleza katika vyuo vya Serikali na kupata madaraja?
(c) Kwa kuwa mitaala ya vyuo vingi imepitwa na wakati, je, Serikali haioni haja ya kuboresha mitaala ya vituo hivyo ili iendane na wakati uliopo kama vyuo vya VETA?
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero imetenga shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununulia vifaa na ukarabati wa Kituo cha Ufundi Stadi Mchombe na shilingi milioni 15 kwa ajili ya kufufua Kituo cha Ufundi Stadi Mpanga. Aidha, Serikali inaendelea kubaini walimu waliosomea fani mbalimbali za ufundi ili wahamishiwe kwenye vituo hivi vya ufundi stadi vikiwemo vituo vya Mchombe na Mpanga.
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wanafunzi wanaohitimu mitihani ya NECTA katika vituo vya ufundi vilivyoko kwenye shule za msingi hawajapatiwa vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo tangu mwaka 2015. Aidha, mitaala inayotumika kutoa mafunzo katika vituo vyote 208 ambavyo kwa mwaka 2018 vina wanafunzi 3,000 na walimu 557 ni ya muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Serikali inaupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaohitimu mafunzo hayo wanapatiwa vyeti ili wavitumie katika michakato ya kujiendeleza au kazi kwani vijana hao ni sehemu ya nguvukazi katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Kwa kutumia uzoefu uliopatikana hadi sasa, Serikali itaifanyia mapitio mitalaa ya mafunzo hayo ili iendane na mahitaji sasa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved