Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 14 | Sitting 2 | Industries and Trade | Wizara ya Viwanda , Biashara na Uwekezaji | 24 | 2019-01-30 |
Name
Khadija Nassir Ali
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Serikali imekuwa ikijitahidi kuvisimamia na kuviwezesha viwanda vyetu vya ndani lakini cha kusikitisha ni kwamba Serikali imeshindwa kusimamia bidhaa zetu ndani ya soko hili huria. Mathalani, bidhaa za viuadudu zinazozalishwa na kiwanda kilichopo Kibaha hazipo sokoni na wananchi hawana uelewa nazo:-
Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuweka fedha kwenye viwanda vyetu bila ya kuwa na mikakati mizuri ya kibiashara ni kuendelea kutumia vibaya fedha za walipa kodi?
Name
Eng. Stella Martin Manyanya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nyasa
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya uwekezaji wowote kufanywa na Serikali, mara zote utafiti na upembuzi yakinifu hufanyika ili kujiridhisha na manufaa ya uwekezaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluwiluwi vya mbu waenezao ugonjwa wa malaria kilichopo TAMCO-Kibaha kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Shirika la Taifa la Maendeleeo (NDC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi mbalimbali zimefanyika katika kutoa elimu kwa wananchi na makampuni ya ndani na nje ya nchi juu ya matumizi ya viuadudu vinavyozalishwa. Uhamasishaji umekuwa ukifanyika kupitia miongozo na jinsi ya kutokomeza viluwiluwi wa mbu waenezao malaria, mikutano, makongamano na hata vipindi vya runinga. Uhamasihaji ulianza mwaka 2015 na kufikia 2018 mwishoni, Halmashauri za Mikoa yote 26 za Tanzania Bara zilikuwa zimenunua viuadudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji umefanyika pia katika nchi za jirani na Jumuiya za Nchi za SADC ambapo katika kikao cha SADC cha Agosti, 2018 nchi hizo ziliazimia kiwanda cha viuadudu kitakuwa msambazaji pekee wa viaududu kwa nchi hizo. Aidha, ili kuwezesha kaya moja moja kutumia viuadudu, kiwanda kimetengeneza vifungashio vidogo vya ujazo wa milimita 30 ambazo bei yake ni Sh.1,000 na vinapatikana kwenye maduka mengi ya dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya uhamasishaji huo ni kuwa jumla ya lita 466,278 za viuadudu zimeshauzwa ambapo lita 269,900 ziliuzwa katika soko la ndani na lita 196,378 ziliuzwa nje ya nchi katika nchi za Niger na Angola. Nchi ya Angola imeonesha nia ya kununua viuadudu vingine lita 85,192 ifikapo mwezi Februali, 2019. Aidha, nchi za Siri Lanka, Serbia, Msumbiji, Rwanda, Kenya na Burundi zimeonesha nia ya kununua viuadudu hivyo na mazungumzo na ufuatiliaji yanaendelea.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved