Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 18 | Sitting 1 | Water and Irrigation | Wizara ya Maji | 11 | 2020-01-28 |
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-
Jimbo la Rombo hususan ukanda wa chini wenye takribani vijiji 41 lina shida ya maji; na Halmashauri imeanzisha mradi wa kupanua bomba kubwa la maji linalotoka Marangu. Aidha, Halmashauri ilipendekeza vyanzo vingine ikiwemo matumizi ya maji na Ziwa Chala, uchimbaji wa visima na mabwawa yatokanayo na mito ya msimu.
(a) Je, Serikali imekubali mpango wa kuanza kutumia maji ya Ziwa Chala?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kutosha ili mradi huo uweze kuanza?
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Roman Selasini, Mbunge wa Jimbo la Rombo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali tayari ina mpango wa kutumia Ziwa Chala kama chanzo cha maji kwa wananchi wa Rombo. Uamuzi huo ulitokana na upembuzi yakinifu na usanifu uliofanyika kuanzia mwezi Machi, 2019 na kukamilika mwezi Julai, 2019. Upembuzi huo ulibainisha vyanzo vinne vya maji ambavyo ni chanzo cha maji cha Ziwa Chala kitakachohudumia vijiji 21 na vyanzo vingine vitatu vya maji vya mtiririko Mto Njoro, Mto Yona na Marangu na Uswai Wambushi.
Mheshimiwa Spika, makisio ya awali ya mradi huo ni shilingi bilioni 40 ambapo ujenzi wake uliamuliwa ufanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza itahusu ujenzi wa chanzo cha maji cha Njoro ambacho kitahudumia Mji wa Tarakea na vijiji jirani na katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi huo Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza na kuanza awamu nyingine.
Mheshimiwa Spika, baada ya awamu zote kukamilika mradi huu unatarajia kuhudumia vijiji vya Kikelelwa, Mbomai, Kibaoni, Nayeme, Nasae, Msanjai, Urauri, Ushiri, Ikuini, Mrao, Kiruakeni, Kisale, Marangu, Mamsera, Mahida, Holili, Mengwe na Ngoyoni vyenye jumla ya watu 157,000.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved