Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Roman Selasini
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Rombo
Primary Question
MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:- Jimbo la Rombo hususan ukanda wa chini wenye takribani vijiji 41 lina shida ya maji; na Halmashauri imeanzisha mradi wa kupanua bomba kubwa la maji linalotoka Marangu. Aidha, Halmashauri ilipendekeza vyanzo vingine ikiwemo matumizi ya maji na Ziwa Chala, uchimbaji wa visima na mabwawa yatokanayo na mito ya msimu. (a) Je, Serikali imekubali mpango wa kuanza kutumia maji ya Ziwa Chala? (b) Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kutosha ili mradi huo uweze kuanza?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Matumizi ya maji ya Ziwa Chala yaliombwa hapa Bungeni na Wabunge wote walionitangulia; Mheshimiwa Alphonce Maskini, Mheshimiwa Aloyce Ngalai, Mheshimiwa Justine Sarakana, Mheshimiwa Basil Pesambili Mramba na Awamu zote Tano za utawala wa nchi hii. Naomba nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano na kuishukuru kwa uamuzi wake wa kuamua kutumia maji haya kwa ajili ya wananchi wa Rombo na nina hakika kama mradi huu utatekelezwa shida ya maji katika Jimbo la Rombo itakuwa ni historia. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kuuliza mradi huu unategemewa kuanza na kumalizika lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi sasa kuna visima viwili ambavyo vimeshakamilika vinatusumbua sana pale Rombo, Kisima cha Leto na Kisima cha Shimbi Mashariki. Namshukuru Naibu Waziri, wiki iliyopita alikuwa Rombo na alitoa maagizo ili haya maji yapate kutumika kwa wananchi.
Sasa swali langu maagizo yamekuwa yanatolewa lakini hayatekelezwi, je, sasa Serikali iko tayari kuwashughulikia maofisa na watendaji ambao wanazuia maji haya yasitumike na kusababisha mateso kwa wananchi?
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli uungwana ni vitendo Mheshimiwa Mbunge ni muungwana. Kutokana na uungwana huo wa kushukuru sisi kama Serikali nataka nimhakikishie tutatekeleza Mradi ule wa Ziwa Chala katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji na mpaka hivi tunavyozungumza tulishatoa agizo kwa maana ya wataalam wetu waweze kufanya makisio na tutawatumia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya uanzaji wa mradi ule ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, la pili nikiri kabisa tuna Mradi wa Leto pamoja na Shimbi Mashariki, nimetoka juzi, moja ya changamoto ulikuwa ni uzembe wa mkandarasi ilihali fedha tumempa. Kwa hiyo tumemwagiza na tumemshughulikia ipasavyo, ndani ya wiki hii maji yale yatafunguliwa na wananchi wako wataweza kupata huduma ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved