Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 29 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 242 | 2016-05-26 |
Name
Neema William Mgaya
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya hifadhi ya Mpanga na wananchi wa Wilaya ya Wanging‟ombe?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uhifadhi katika hifadhi ya Mpanga Kipengele ulianzishwa za Tangazo la Serikali (GN) Na. 483 la tarehe 25 Oktoba, 2002 ambapo eneo lililoidhinishwa lilitangwazwa kuwa pori la akiba kwa maslahi mapana ya Kitaifa. Uhifadhi wa eneo hili unahusisha utunzaji wa rasilimali zinazotoa fursa ya utalii, matumizi ya kiikolojia na vyanzo vya maji kupitia mito ya Mbarali, Mlomboji, Kimani na Ipera ambayo kwa pamoja huchangia maji ya mtoa Ruaha Mkuu, ambao ni muhimu kwa shughuli za kilimo ikiwemo umwagiliaji wa mashamba, mahitaji ya watu na uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Wilaya za Makete na Mbarali, poli la akiba Mpanga na Kipengere limepatikana na takribani Vijiji kumi vya Wilaya ya Wanging‟ombe ambapo chanzo cha mgogoro ni wananchi wa Vijiji vinne ambavyo viko ndani ya mpaka wa hifadhi, na vingine vinne nje wa mpaka wa hifadhi kukataa kutambua mipaka iliyowekwa na Tangazo la Serikali na hivyo kugoma kuhama kupisha shughuli za uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro huu na eneo lote linalozunguka pori hili, Wizara yangu ilifanya vikao vya majadiliano na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Makete tarehe 20 mpaka 21, Novemba, 2014; Wanging‟ombe tarehe 26 mpaka 27, Novemba 2014 na Wilaya Mbarali tarehe 26 mpaka 27, Februari, 2015 na hatimaye kufanyika kwa tathmini kutambua idadi ya wananchi na mali zao zisizohamishika na uthamini wa kiasi cha fedha kitakachohitajika kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uthamini uliofanyika mwaka 2007 na 2012 katika Wilaya ya Makete mwaka 2007, wananchi 325 wa Vijiji vya Ikovo, Usalimwani na Kigunga vya Wilaya ya Makete walilipwa fidia ya shilingi 190,067,151. Mwaka 2012 wananchi 161 wa Kijiji cha Ikovo walilalamikia kupunjwa, hivyo uthamini wa ardhi na gharama za kuhama ulifanyika tena ambapo walilipwa jumla ya shilingi 829,841,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika tathmini iliyofuata iliyofanyika na kukamilika mwaka 2015 Wilayani Mbarali, wananchi 308 katika Kitongoji cha Machimbo, Kijiji cha Mabadaga wanategemewa kulipwa jumla ya shilingi 717,650,000 katika mwaka wa fedha 2016/17. Tathmini na uthamini kwa Vijiji vya Wilaya ya Wanging‟ombe imepangwa kufanyika kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu, wavumilivu na kuepukana na shughuli ambazo zinaweza kuleta athari katika maeneo hayo muhimu kwa Taifa letu, kwani Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutatua changamoto za migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na ya wananchi. Vilevile tunahimiza Mkoa, Halmashauri za Wilaya na Waheshimiwa Wabunge washirikiane na Wizara kuhamasisha elimu ya uhifadhi na pia kuwashawishi wananchi kukubali kuhama na kupisha uhifadhi mara baada ya taratibu kukamilika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved