Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 2 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 19 2019-09-04

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-

Baadhi ya mechi za mpira wa miguu za Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019 zilichezwa bila kuwepo kwa gari la wagonjwa uwanjani na kusababisha wachezaji walioumia kulazimika kukimbizwa Hospitali kwa kutumia magari ya kawaida:-

(a) Je, Serikali ina taarifa juu ya tatizo hilo?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kosa hilo halitokei tena viwanjani?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu na sharti la kuwepo kwa magari ya wagonjwa viwanjani ili kuhudumia wachezaji na hata watazamaji wanaopatwa na dharura kubwa za kiafya na dharura inayohitaji huduma haraka ya matibabu. Aidha, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) linaheshimu Kanuni hiyo pamoja na kwamba utekelezaji wake katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu unakawamishwa na uhaba wa magari ya wagonjwa ambayo huchelewa kufika uwanjani siyo kwa makusudi bali ni kwa kutingwa na huduma zingine za tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, ni mechi ya Mbao FC dhidi ya Coastal Union iliyochezwa katika Uwanja wa CCM-Kirumba ambapo mchezaji aliumia kipindi cha kwanza lakini gari la kubebea wagonjwa lilikuja kipindi cha pili kutokana na gari hilo kuwa na majukumu mengine Mkoani hapo. Hali hii inasababishwa na ukweli kwamba hakuna Chama cha Soka cha Mkoa kinachomiliki magari ya wagonjwa, magari yote yanapatikana kwenye Halmashauri husika, baadhi ya hospitali za Serikali na asasi zenye magari ya wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, natoa wito kwa Kamati za Michezo za Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na mamlaka nilizozitaja kwenye huduma hii ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa kukosa huduma hiyo inapohitajika. Aidha, nawahimiza TFF na uongozi wake wa Mikoa kujiongeza kwa kufikiria njia rahisi zaidi za kubebea majeruhi kama vile pikipiki maalum za miguu mitatu au miwili kwenye mechi za ligi ya chini ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea kwa majeruhi kucheleweshwa kupelekwa hospitalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.