Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:- Baadhi ya mechi za mpira wa miguu za Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/2019 zilichezwa bila kuwepo kwa gari la wagonjwa uwanjani na kusababisha wachezaji walioumia kulazimika kukimbizwa Hospitali kwa kutumia magari ya kawaida:- (a) Je, Serikali ina taarifa juu ya tatizo hilo? (b) Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kosa hilo halitokei tena viwanjani?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali hata hivyo bado kuna changamoto mbili, tatu. Kwa mfano, madaktari wote wanaojitambulisha kama madaktari wa timu wanapokwenda na timu uwanjani, wengi siyo madaktari ni mashabiki tu ambao wanebeba hiyo mikoba ya first aid na hii ni hatari kwamba inapotokea matatizo wanakuwa hawana utalaam wa kutoa huduma ya kwanza viwanjani. Je, Serikali itakuwa tayari kuwashauri sasa TFF na Bodi ya Ligi kuwatambua madaktari wenye sifa ndiyo wapewe hiyo nafasi ya udaktari wa kuingia na timu viwanjani? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wachezaji wengi hawana bima za afya jambo ambalo linapelekea wanashindwa kujituma mazoezini na viwanjani kwa kuhofia kuumia. Serikali itakuwa tayari kuwashauri pia TFF badala ya kupoteza muda mwingi kuchunguza Makocha wamevaa nini sasa wakaongee na mashirika ya bima za afya ili waweze kuwapa bima za afya wachezaji?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa ni mdau mkubwa sana wa michezo na hivi majuzi


tumeshuhudia timu yake ya Umoja wa Vijana wa Temeke ikishinda kwenye Mashindano ya Ndondo Cup kwa msimu wa mwaka 2019. Kwa hiyo, hongera sana Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya msingi amezungumzia suala zima la madaktari wa timu kwamba wengi wa madaktari wa timu hawana vigezo au sifa za kuwa madaktari. Suala la timu zote kuwa na madaktari ni takwa la kikanuni. Nitumie fursa hii kwanza kuwataka wasimamizi wote wa vilabu nchini Tanzania kuhakikisha kwamba wanatumia madaktari ambao wana sifa za kuwa madaktari kwa sababu tunajua kwamba yako matatizo mbalimbali ambayo huwa yanawapata wachezaji pindi wanapokuwa kwenye mazoezi na kwenye michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Mbunge ametaka tuwashauri TFF wanatambua na kuhakikisha kwamba vilabu vyote vinakuwa na madaktari ambao wana sifa. Nitumie fursa hii kuwataka TFF kuhakikisha kwamba suala hili kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba ni vyema wakasimamia kuhakikisha kwamba vilabu vyote vinakuwa na madaktari wenye sifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili ametaka kujua kuhusiana na bima za afya. Suala la afya za wachezaji sisi kama Wizara tunalisimamia na ndiyo maana kwenye mashindano yote tunahakikisha kwamba kabla wachezaji hawajaenda kwenye mashindano wanapima afya zao. Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua kwamba kwa nini sisi kama Serikali tusiwashauri TFF waongee na mashirika ya bima za afya ili wachezaji waweze kupatiwa bima za afya, ushauri huu mzuri na sisi kama Wizara tumeupokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba TFF wameuchukua na wataufanyia kazi kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba kuhakikisha kwamba wachezaji wote wanakuwa na bima za afya. Suala la bima ya afya siyo tu wachezaji peke yake ni Watanzania wote na tumeona namna ambavyo Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba bima ya afya inakuwa jambo la msingi kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.