Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 2 Home Affairs Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi 29 2019-09-04

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-

Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya watoto wachanga kutupwa majalalani, mitaroni na katika mifuko ya rambo:-

(a) Je, nini kauli ya Serikali kuhusu matukio hayo?

(b) Je, ni watuhumiwa wangapi walishakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria?

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vya kutupa watoto majalalani, mitaroni na maeneo mengine ni kinyume na sheria za nchi na haki za binadamu. Kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 chini ya kifungu cha 218 na 219, adhabu ya makosa hayo ni kifungo cha maisha. Aidha, Serikali inalaani vikali vitendo hivyo na itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaopatikana na hatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za matukio ya kutupa watoto wachanga zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni, 2019 kumekuwa na jumla ya matukio 66 ya watoto waliopatikana wakiwa wametupwa, 43 kati yao waliokutwa hai na 23 walikutwa wamefariki. Aidha, watuhumiwa 18 walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.