Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 22 | Natural Resources and Tourism | Wizara ya Maliasili na Utalii | 191 | 2016-05-18 |
Name
Hassan Selemani Kaunje
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lindi Mjini
Primary Question
MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:-
Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020, imeeleza juu ya uendelezaji wa utalii kwa Ukanda wa Kusini kama Program Maalum:-
Je, ni lini Serikali imepanga kuanza mpango huo maalum?
Name
Eng. Ramo Matala Makani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduru Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2015 - 2020, Sura ya Pili katika aya ya 29 imeainisha program maalum ya uendelezaji wa utalii nchini ikiwemo katika Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano yenye dhamana ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi imeandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia 2016/2017 - 2020/2021 ambao ni sehemu ya pili ya Mpango Elekezi wa miaka 15, (2011/2012 – 2025/2026) na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mpango huo wa miaka mitano, Serikali imejumuisha hatua ya kufungua fursa za utalii katika Ukanda wa Kusini kama mojawapo ya hatua muhimu kwa maendeleo ya viwanda na ukuzaji wa uchumi. Ili kutekeleza azma hii, Wizara yangu imejipanga kushirikisha sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu ya utalii, kuwekeza na kuendeleza maeneo mengine yenye fursa za utalii, kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa Utangazaji wa utalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi, kutoa mafunzo ya ukufunzi katika Chuo cha Taifa cha Utalii kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya Utalii na kutenga maeneo maalum ya utalii, hususan ya fukwe za bahari na maziwa kwa ajili ya hoteli za kitalii kama maeneo muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho, Serikali itashirikisha sekta binafsi ili iwekeze katika kuboresha miundombinu na vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini na kuvitangaza hususan maeneo ya utalii wa kihistoria na kitamaduni kama vile mji wa kihistoria wa Mikindani, Kilwa Kivinje, Pori la Akiba Lukwika-Lumesule na Pori la Akiba la Selous upande wa kusini na maeneo mengine katika Ukanda huo. Aidha, ili kukuza utalii wa baharini na katika fukwe za bahari, Serikali imepanga kutenga maeneo maalum ya utalii hususan kwa ajili ya hoteli za kitalii kando ya Bahari ya Hindi Mkoani Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upana wake, utalii wa Kusini unatarajiwa pia kuboreshwa kupitia program na miradi mbalimbali kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na mradi ujulikanao kama REGROW unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Dola za Kimarekani zisizopungua milioni 100.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved